March 25, 2016

TAMBWE NA KIIZA...

Kasi ya kuwania tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara imeendelea kushika kasi hata nje ya uwanja ambapo kuna kampeni maalum ya kuhakikisha tuzo hiyo inaenda kwa mchezaji fulani.

Mpaka sasa Hamis Kiiza wa Simba ndiye anayeongoza kwa kuwa na mabao 19, akifuatiwa na Amissi Tambwe wa Yanga ambaye ana mabao 17, lakini wachezaji wa Yanga wamesema kuwa wanachotaka ni kufanya juu chini mchezaji mwenzao ampiku Kiiza na kutwaa tuzo hiyo.

Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva amesema wamekubaliana kuongeza nguvu uwanjani na kumtengenezea zaidi Tambwe ili afunge na kuiwezesha timu yake kushinda na yeye kuwa mfungaji bora.

“Mimi nilikuwa mfungaji bora msimu uliopita, Tambwe amefikia idadi hiyo ambayo niliifikia msimu huo, kwangu mimi hakuna tatizo katika hilo, kikubwa ni kuwa tutahakikisha tunamsaidia Tambwe aweze kufanikiwa kuibuka mfungaji bora.

“Tumekubaliana wachezaji wote kuhakikisha tunampatia yeye pasi za mwisho pale atakapokuwa vizuri ili kuweza kufanikiwa kufunga na kuongeza idadi ya mabao yatakayomsaidia kusonga mbele.


“Tunafanya kazi kwa ushirikiano kwani lengo letu ni kuona tunafanikiwa kutwaa ubingwa na kiatu hivyo kila mmoja yupo katika kumsaidia Tambwe,” alisema Msuva. 

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV