April 25, 2016

JUMA ABDUL (KULIA)...
Beki wa pembeni wa Yanga ambaye amekuwa kwenye ubora wa aina yake msimu huu, Juma Abdul, mawazo yake tayari yameshahama, yupo Bongo lakini akili yake yote ipo Ulaya akifikiria na yeye kwenda huko akafanikiwe kama alivyofanikiwa Mtanzania, Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji katika Klabu ya KRC Genk.

Juma Abdul alitamba kwenye mechi ya pili ya Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly nchini Misri na ndiye aliyepiga krosi maridadi iliyozaa bao lililofungwa na Donald Ngoma.

Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa na ambayo wachezaji wa Yanga walicheza soka safi na la kuvutia lililowafurahisha vilivyo mashabiki wa timu hiyo, ilifungwa mabao 2-1 na kujikuta ikitupwa nje ya michuano hiyo.

Juma, baada ya kujiridhisha na kiwango chake msimu huu, amedai kuwa sasa ni wakati wake wa kwenda kusaka maisha bora barani Ulaya kama ilivyo kwa Samatta ambaye anafanya vizuri sasa na kikosi cha KRC Genk.

Juma alisema kuwa hapo awali alikuwa anajiona kama vile bado hajakomaa vizuri kuweza kukabiliana na changamoto za ushindani huko Ulaya lakini kwa sasa yupo tayari kwa kila kitu.

“Siyo mimi tu ambaye nataka kuondoka kwenda kutafuta maisha bora Ulaya ila wapo na wachezaji wengine hapa Yanga wenye ndoto hizo kwa sababu hivi sasa tunajiona kuwa tumekomaa na tunaweza kupambana na wachezaji wa mataifa mengine kuwania nafasi.

“Kiwango tulichoonyesha dhidi ya Al Ahly hicho ndiyo kipimo kizuri kwetu kuwa tunaweza kucheza Ulaya, hivyo huu ndiyo wakati wetu sasa wa kutimiza ndoto zetu, tunawaomba Yanga watupatie nafasi hiyo,” alisema Abdul ambaye alidai kuwa baada ya mechi dhidi ya Al Ahly, kuna mawakala walimfuata na kuzungumza naye na sasa wapo katika harakati za kuhakikisha anatimkia huko alipo Samatta ambaye analipwa euro 35,600 (sawa na Sh milioni 86) kwa mwezi.


Juma Abdul amekuwa na sifa ya uimara katika ulinzi, kupiga chenga na kupiga mashuti ya mbali ambayo mengi yamekuwa yakizaa mabao. Ana mabao mawili kwenye Ligi Kuu Bara. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV