April 16, 2016


Baada ya Yanga kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, leo Jumamosi, beki na nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amewashukuru mashabiki waliojitokea uwanjani hapo kuwashuhudia lakini akasema kuwa akili yao yote sasa ni kwa Waarabu wa Al Ahly.

Yanga imepata ushindi huo na sasa inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 59 ikifuatiwa na Simba ambayo ina pointi 57 zote zikiwa zimecheza mechi 24 na kusaliwa na michezo sita kabla ya kumaliza msimu hu.

Cannavaro ambaye alikuwemo kwenye kikosi hicho cha leo, amesema kuwa ushindi huo ni mzuri na umeongeza hamasa kwao kuelekea mchezo huo wa Ligi ya mabingwa Afrika ambapo ni mchezo wa marudio wa raundi ya pili ya michuabno hiyo.

“Ushindi huu ni muhimu sana kwetu, tumefurahi na tunashukuru mashabiki, sasa hatuifikirii ligi kuu kwa sasa wa kuwa tunajua mchezo ulio mbele yetu ni mkubwa na muhimu, hivyo tutapambana kuhakikisha tunasonga mbele, tunajua Al Ahly ni timu nzuri na hilo linajulikana kwa kila mtu lakini sasa tunaenda kujiandaa kwa ajili ya mchezo huo,” alisema Cannavaro huku akionekana mwenye furaha.Katika mchezo uliopita baina ya Yanga dhidi ya Al Ahly uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, wiki iliyopita timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, ambapo zinatarajiwa kurudiana Jumatano Aprili 20, 2016 nchini Misri.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV