April 16, 2016UNAWEZAJE kuikosa hii kwanza!  Lile tamasha la kila mwaka lenye lengo la kuibua vipaji vya michezo na kumuinua Mtanzania wa kipato cha chini, Majimaji Selebuka limewadia tena.

Tamasha hilo ambalo huratibiwa mjini Songea, Ruvuma kila mwaka, safari hii limepangwa kufanyika kati ya Mei 28 mpaka Juni 4, mwaka huu huku maandalizi yakiwa yamekamilika kwa kiasi kikubwa.

Katika mahojiano maalumu na mratibu wa tamasha hilo, Reinafrida Rwezaura amesema tofauti na mwaka jana, tamasha la mwaka huu kuna mwitikio mkubwa sana.
  
Maandalizi:
Tayari kampuni tano zimekubali kudhamini tamasha hilo huku wakitarajiwa kuwa na washiriki kutoka nchi jirani.
“Tunashukuru mpaka sasa muitikio ni mkubwa, kuna kampuni kama tano zimekubali kutudhamini na nyingine bado tuko kwenye mazungumzo.

“Tofauti na mwaka jana, safari hii watu wamejitokeza kwa wingi mno na tunatarajia kuwa na washiriki kutoka nje ya nchi kama vile Zambia, Msumbiji na Malawi ambao watashiriki katika michezo mbalimbali,” anasema.


Shughuli zitakazokuwepo
“Kutakuwa na mgawanyo wa shughuli. Tuna michezo pamoja na shughuli za kijamii mfano, maonyesho ya ujasiriamali na biashara, utalii wa ndani kama vile Hifadhi ya Ruhira, Misitu ya Kongore na Matogoro, Makumbusho ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji pamoja na midahalo (debate) kwa shule za sekondari na mpaka sasa shule 20 zimethibitisha kushiriki.

“Pia tutakuwa na michezo kama ngoma za asili, mbio za baiskeli KM 50 (kutoka Songea mjini mpaka Peramiho), riadha za KM 42, 21, 10 na KM 5 ambazo zitakuwa ni za kujifurahisha.”

Washiriki ni akina nani?
Reinafrida anasema: “Ni kila mtu lakini lazima atimize vigezo. Awe na miaka kuanzia 18 na kuendelea, awe na uzoefu wa kutosha katika kila fani atakayoona inamfaa na pia kutakuwa na viingilio vya ushiriki lakini vinatofautiana.
“Baiskeli na ngoma za asili ada ya ushiriki ni Sh 10,000, vikundi vya ujasiriamali kwa wakazi wa Ruvuma ni Sh 50,000  ambayo ni ada ya wiki nzima katika kuuza na kutangaza bidhaa zao na Sh 60,000 kwa kikundi kutoka nje ya mkoa huo, pia kwa mjasiriamali mmojammoja, ada yake ni Sh 15,000.

“Pia ushiriki wa riadha KM 42 ni Sh 10,000, KM 21 (Sh 5000), KM 10 (Sh 3000) wakati zile za KM 5 ni bure.” 


Aidha, kutakuwa na vyeti kwa washiriki wote pamoja na medali na zawadi kwa washindi katika kila kategori.
Usaili kwa ajili ya vikundi vya ujasiriamali utafanyika wiki moja kabla ya kuanza kwa tamasha hilo, tayari vikundi 10 vilivyoshiriki mwaka jana vimethibitisha kushiriki tena mwaka huu.


Majimaji Selebuka ni nini?
Ni tamasha linaloratibiwa na Asasi ya isiyo ya kiserikali ya SOMI (Songea & Mississippi) iliyoanzishwa mwaka 2007. Lengo kuu ikiwa ni kuendeleza uhusiano na urafiki mwema wa kimaendeleo kati ya majimbo mawili; Songea ya Tanzania na Mississippi ya Marekani.

Mbali na urafiki pia hutoa fursa kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma hasa Wilaya ya Songea kuonyesha vipaji vyao kuanzia michezo, elimu na shughuli za kijamii.

Tujikumbushe ya mwaka jana
Mbio kwa wanaume – Km 5, Km 21  & Km 42
Bingwa wa mbio fupi KM 5 alikuwa Ronaldo Sumwa, KM 21 (Mohammed Dule) na zile za KM 42 alikuwa Paul Modest.

Ngoma za Asili: Kikundi cha Jakaya Sanaa Group kiliibuka kidedea kwa kuvipiku vikundi vya Lihanje, Ligambusa Beta Group, Beta Tawi la Amani, Londoni, Ngoma ya Mganda na Kioda.


Mbali na medali na zawadi kwa washindi, pia kikundi cha Jakaya kilipewa ofa ya kurekodi CD 100 bure katika moja studio za kisasa hapa nchini.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV