April 25, 2016


Na Saleh Ally
WACHEZAJI wa Coastal Union jana walikuwa uwanjani katika mechi ya nusu fainali dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga.

Hii ilikuwa ni mechi ya Kombe la FA la Azam Sports HD hatua ya nusu fainali na kipindi chote cha kwanza Coastal Union wakatawala vilivyo mchezo huo.

Coastal Union ni kati ya timu zenye wachezaji wengi sana vijana. Wachezaji ambao baadhi yao walionekana hawafai katika timu nyingine, wamekuwa mashujaa wakiwa Coastal Union.

Coastal Union iliishaifunga Yanga katika mechi ya Ligi kuu Bara, ikafanya hivyo kwa kuitwanga Azam FC pia. Hii ndiyo timu iliyozifunga Azam na Yanga kwa pamoja.

Kama hiyo haitoshi, Coastal Union ikaonyesha inaweza kuwamaliza vigogo baada ya kuitwanga Simba katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho.

Kama utapiga hesabu za kawaida kabisa, Coastal Union ndiyo timu pekee iliyozifunga timu zote tatu vigogo yaani, Yanga, Simba na Azam FC. Unaweza kuwaita kiboko cha vigogo.

Hata katika mechi ya jana ya nusu fainali ya Kombe la FA, Coastal Union ndiyo iliyoonyesha soka la kuvutia na kuiweka Yanga katika wakati mgumu muda wote.

Ukitaka kuwa ‘fea’, angalia bao la Coastal Union, alilofunga Yossouf Sabo, halafu angalia mabao mawili ya Yanga aliyofunga Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambaye alisukuma mpira wavuni kwa mkono.

Hii inaonyesha kabisa, Coastal Union wako vizuri na wana timu bora sana. Huenda ingekuwa nadra kwa Yanga kushinda jana kama waamuzi wangekuwa wamechezesha mpira vizuri na kuzingatia sheria 17 kwa usahihi.

Achana na ubovu wa waamuzi, tuendelee kuzungumzia kikosi cha Coastal Union namna ambavyo kimekuwa ndiyo chenye njaa kuliko kingine chochote cha Ligi Kuu Bara.

Lakini ndicho kimewafunga vigogo wote. Picha inasema hivi, Coastal Union ina kikosi bora cha vijana kuliko timu yoyote ya Ligi Kuu Bara na huenda ilikuwa na kikosi bora katika Kombe la FA.

Wachezaji wake wana sura za sasa, vijana wa enzi za Jakaya Kikwete wenye mioyo ya enzi za Julius Kambarage Nyerere. Utakumbuka wachezaji wa zamani walikuwa hawalipwi fedha nyingi lakini walipambana vilivyo na kuzifikisha timu zao mbali.

Hata timu ya taifa, ilicheza Kombe la mataifa Afrika mara ya kwanza na mwisho mwaka 1980. Ndiyo enzi hizo za Nyerere, wachezaji walilipwa kiduchu na wakafanya vema kabisa.  Lakini wachezaji wa sasa wanalipwa fedha kibao, lakini hawana kitu.

Vijana wa Coastal Union wamekuwa na mioyo ya upambanaji, walitaka kufanya vema lakini wakaangushwa na viongozi wabovu waliokuwa nao, ambao hawakuwa na malengo na waliona uongozi ni kama sehemu ya kuringishia au kuonyesha na wapate nafasi ya kujitapa mitaani.

Huenda Tanga ungekuwa mkoa wenye ushirikiano mkubwa. Basi bila shaka Coastal ilikuwa na nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa kuwa bingwa wa Bara au Kombe la FA.

Viongozi wengi ndiyo sumu ya michezo nchini. Kwenye soka ndiyo usiseme maana wamekuwa wanasiasa zaidi kuliko kuwa wanamichezo na utendaji wao ni midomoni zaidi kuliko matendo ya utekelezaji kwa vitendo sahihi.

Kuna jambo la kujifunza, walichokionyesha vijana wa Coastal Union kwamba njaa haiwezi kuzuia mafanikio ya mtu au watu wanaotaka kufanikiwa.
Lakini ni mfano mwingine kwa viongozi wajanjawajanja na wababaishaji kama waliokuwa kwenye uongozi wa Coastal Union. Kwamba wanaukwamisha mpira kwa matakwa yao binafsi.



1 COMMENTS:

  1. Timu inayopigana kushuka kutoswhuka daraja!? kweli mapenzi yakizidi ni shida!!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic