April 11, 2016

KANU AKIWA NA SALEH ALLY 'JEMBE' MUDA MCHACHE BAADA YA MAHOJIANO..

 Na Saleh Ally
UNAPOKUTANA na Nwankwo Kanu, unakuwa umekutana na mwanasoka kati ya wachache sana barani Afrika ambao ‘wananuka’ makombe makubwa ambayo wachezaji wengi maarufu wa barani Ulaya au Amerika Kusini wamekuwa wakiyasikia tu.

Kanu amebeba ubingwa wa Uholanzi mara tatu, Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Ajax pamoja na Uefa Super Cup. 

Mshambuliaji huyo wa Nigeria, pia amebeba ubingwa wa England mara mbili akiwa na Arsenal chini ya Arsene Wenger, pia akachukua ubingwa wa FA Cup mara mbili. Safari ya kwanza akiwa na Arsenal halafu Portsmouth. Usisahau Ngao ya Jamii akiwa na Arsenal tena.

Najua unakumbuka mwaka 1996 alipokuwa nahodha wa Nigeria iliyobeba ubingwa wa Olimpiki kwa kuzikaanga Argentina na Brazil katika nusu fainali na fainali. Hakika ni mchezaji mkubwa mwenye rekodi kubwa na anayeheshimika.

Usisahau Kanu ni mwanasoka bora wa BBC mara mbili (1997 na 1999). Pia ni mwanasoka bora Afrika mara mbili (1996 na 1999).

Kanu ambaye sasa ni Balozi wa StarTimes barani Afrika, yupo nchini kwa ziara ya siku kadhaa na tayari ametembelea sehemu mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, zaidi akihakikisha anafika katika wodi ya wagonjwa wa moyo, tatizo lililowahi kumkumba akiwa Inter Milan, lakini Mungu akamsaidia, matibabu yakawa mazuri na akapiga soka kwa miaka zaidi ya 15 hadi alipostaafu.


Katika mahojiano na Kanu ili kujua mambo kadhaa ambayo alipitia katika maisha yake ya soka.
SALEHJEMBE: Unawaonaje Watanzania?
Kanu: Ni watu wacheshi, nimepapenda sana Tanzania, nasikia faraja pia.

SALEHJEMBE: Pole kwa kuwa ulipata matatizo ya moyo, unashauri nini katika hili?
Kanu: Najua Afrika hatuna vifaa sahihi kwa ajili ya vipimo kwani ni ghali sana. Lakini vizuri watu waangalie afya zao kwa kuwa huwezi kujua.

SALEHJEMBE: Mara ya kwanza ulipogundua una ugonjwa wa moyo, ilikuwaje? Ulifikiria utachezaje?
Kanu: Nilishtuka sana, ndugu, rafiki na wachezaji wenzangu wakanipa matumaini. Kawaida sikufikiria sana kucheza, badala yake niliwaza kuhusiana na kuachana na mpira na kujitibu. Pia nilianza kuwafikiria watoto wa Afrika, ndiyo maana baada ya kustaafu naendelea kupambana. Lazima tutafute namna ya kuwasaidia.


SALEHJEMBE: Namna gani sasa?
Kanu: Mfano kutafuta fedha za matibabu. Mfano kucheza mechi za kirafiki, kuandaa matamasha. Hivi ndivyo namna taasisi yangu inavyofanya kazi.

SALEHJEMBE: Ni jambo zuri, tukirudi kwenye soka, nini tatizo la Afrika? Kuna vipaji lakini mafanikio ni tatizo!
Kanu: Afrika ni sawa na Brazil unapozungumzia vipaji. Tatizo ni maandalizi na uongozi.

SALEHJEMBE: Uongozi kivipi?
Kanu: Wengi si wakweli, hawapo tayari kwa ajili ya mpira, pia wengi hawajacheza mpira.

SALEHJEMBE: Unafikiri wachezaji wanafaa kuwa viongozi?
Kanu: Kabisa, itakuwa vizuri kwa kuwa watafanya kazi wakijua kila kitu kuanzia maumivu na raha ya mchezaji.

SALEHJEMBE: Lakini wengi wanaonekana ni waoga!
Kanu: Hawana sababu ya kuwa waoga, waende tu wakapambane kwa ajili ya mpira.


SALEHJEMBE: Katika mechi zako, ipi inabaki kuwa kumbukumbu kuu?
Kanu: Ziko nyingi sana kwa kweli. Lakini kawaida kabisa nitasema mechi dhidi ya Brazil katika Olimpiki, hakikuwa kitu kidogo.

SALEHJEMBE: Unaweza kuelezea kidogo?
Kanu: Kukutana na timu yenye wachezaji kama Ronaldo de Lima, Rivaldo, Bebeto, Roberto Carlos halafu mnawafunga. Si kitu kidogo.


SALEHJEMBE:Ulianza kuvaa namba nne ukiwa mshambuliaji, ilikuwaje?
Kanu: Kuna kabila moja Nigeria wanaamini namba nne ina baraka. Nikaamua nipate hizo baraka.

SALEHJEMBE: Unakubali ulifanya mapinduzi, washambuliaji wakaanza kuamini namba za chini ambazo zilionekana za mabeki?
Kanu: Kabisa, washambuliaji walianza kuona kawaida kuvaa namba nne. Wengine wakabuni tatu, tano na kadhalika. Ni jambo zuri kuanzisha kitu na wengine wakafuata.


SALEHJEMBE: Ukiangalia timu yako ya zamani ya Arsenal inavyokwenda, huoni ni wakati mwafaka wa Wenger kuondoka?
Kanu: Kwanza sioni kocha gani atachukua nafasi yake. Lakini ajiuzulu sawa, Arsenal wamejiandaa?

SALEHJEMBE: Kipindi kile, Arsenal mlipambana na kubeba ubingwa, sasa ubingwa wa England kwa Arsenal ni hadithi, unafikiri kwa nini?
Kanu: Watu waliokuwepo kwenye timu mfano Patrick Vieira, Tony Adams na wengine walikuwa ni watu wanaotaka ubingwa. Aina ya watu wanaotaka kushinda na wanatekeleza. Sasa ni tofauti kidogo, ingawa bado Arsenal ina nafasi.


SALEHJEMBE: Enzi zako England, beki gani alikutisha?
Kanu: Kweli sikumbuki, nilipenda mimi ndiyo niwatishe mabeki badala ya kuwaogopa.

SALEHJEMBE: Ukizungumzia fowadi ambaye hadi leo unamkubali, nani kwako ni kiboko?
Kanu: Ronaldo wa Brazil, nilicheza naye Inter Milan. Huyu mtu anajua mpira, kuanzia kutuliza, kukimbia nao, mbinu na hata kufunga. Lakini Denis Bergkamp, ni mtu mwingine wa aina yake.


SALEHJEMBE:Unafikiri Nigeria ina wachezaji watakaokuja kuwa tishio kama enzi zenu?
Kanu: Wako wengi, hiki ni kipindi wanakua. Mmoja wao ni (Alex) Iwobi wa Arsenal.

SALEHJEMBE: Ushindani wa sasa umebaki kwa Messi na Ronaldo. Wakati wenu wachezaji walikuwa wengi, unaona hili ni sawa?
Kanu: Kweli hata mimi sifurahii sana, hata Afrika umeona Yaya (Toure) amechukua mara nne mfululizo. Ushindani unatakiwa zaidi.


SALEHJEMBE: Messi na Ronaldo, nani anakuvutia zaidi?
Kanu: Wote, wale kila mtu ana aina yake ya uchezaji na ana mvuto wake.

SALEHJEMBE: Miaka yako mitano Arsenal ukiwa umecheza mechi 119 na mabao 30, unamzungumzia Wenger kama mtu wa aina gani?
Kanu: Wenger kama unavyomuona, ni mtaratibu sana. Sijawahi kumsikia akipayuka kwa hasira. Hata kama mmeharibu, akiingia vyumbani wakati wa mapumziko au baada ya mechi, atazungumza vizuri kwa kuwaelewesha vizuri tena bila kelele hata kidogo.


SALEHJEMBE: Unapenda muziki wa aina gani?
Kanu: Napenda sana Hip Hop za Kinigeria!

SALEHJEMBE: Wasanii wanaokuvutia?
Kanu: Wiz Kid, P Square na wengine.

SALEHJEMBE: Tafadhali nitajie wimbo mmoja tu unaokuvutia zaidi.
Kanu: No Easy wa P Square (anaimba mistari kidogo). Wanazungumzia maisha si rahisi. Kweli, ni wimbo mzuri sana.

SALEHJEMBE: Kwa kuwa una majukumu mengine, nashukuru sana kwa ushirikiano ukiwa Balozi wa StarTimes Afrika nzima, kila la kheri kuendelea kuiwakilisha kampuni hiyo maarufu  ya ving’amuzi vinavyopendwa.
Kanu: Nashukuru sana.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic