April 29, 2016Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, juzi Jumatano alitangaza kuwa huu sasa ni muda wa vita klabuni kwake kwa kuwa anachotaka ni ushindi tu bila kujali kiwango kinachoonyeshwa na timu yake.

Kauli hiyo inakuja wakati ambapo Yanga imesaliwa na michezo mitano kumaliza msimu wa Ligi Kuu Bara na ipo kileleni ikifuatiwa na Azam na Simba.

Pluijm amefikia hatua hiyo baada ya timu yake kupata ushindi kwa tabu wa mabao 2-1 katika mchezo wa juzi dhidi ya Mgambo kwenye Uwanja wa Taifa.

“Kuanzia leo (juzi) hatuna tena mechi ya ligi kuu msimu huu kwenye Uwanja wa Taifa, mechi zote tulizobakiza ni za ugenini ambazo naamini zitakuwa na changamoto kubwa kwetu lakini nimejipanga kwa kila kitu.

“Nimeshazungumza na wachezaji wangu juu ya suala hilo na kuwataka kila mmoja kuhakikisha anapambana kwa faida ya timu lakini pia natarajia kubadili mbinu za uchezaji kutokana na aina ya viwanja tunavyokwenda kukutana navyo.

“Hivi sasa tutalazimika kuachana na soka la pasi fupifupi na badala yake tutakuwa tukitumia mipira mirefu ambayo tutatakiwa kuicheza kwa ufanisi mkubwa ili tuweze kupata matokeo mazuri,” alisema Pluijm.

Michezo ambayo Yanga imesaliwa nayo katika Ligi Kuu Bara ni dhidi ya Toto Africans ambayo itachezwa Mwanza, Stand United (Shinyanga), Mbeya City (Mbeya), Majimaji (Songea) na Ndanda FC (Mtwara).

Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi 62 ikifuatiwa na Azam FC 58, Simba 57, Mtibwa Sugar 43 na Prisons 41.


1 COMMENTS:

  1. Hayo ndio maneno.Haijalishi mpira ni wa aina gani kinachotakiwa ni ushindi tu.Kwa wale wajasiriamali usisahau pia kupitia MUKEBEZI BLOG au bonyeza hapa shareinfogrouptanzania.blogspot.com

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV