April 29, 2016


Na Saleh Ally
UKIACHANA na mechi ya kesho wakati Yanga itakuwa inapambana na Toto Africans jijini Mwanza, nne zilizobaki zinaweza kuwa ngumu zaidi kwa Yanga, hasa kama wanachama wake hawatakuwa makini, nitakueleza kwa nini.
Kwanza, nikukumbushe ratiba halisi ilivyo. Ndani ya mwezi wa tano, Yanga itacheza mechi zake nne zilizobaki za Ligi Kuu Bara ambazo zitaamua kama inaweza kuwa bingwa au la.

Angalau ishinde mechi mbili kati ya hizo nne, inaweza ikawa imejihakikishia ubingwa kwa asilimia 90.

Mechi ya kwanza kati ya hizo nne ni Mei 3 dhidi ya Stand United ikiwa ugenini mjini Shinyanga, pili ni Mei 10 dhidi ya Mbeya City ikiwa ugenini Mbeya, Mei 15 kazini tena dhidi ya Ndanda na mwisho ni Mei 21 itakapomaliza mechi ya mwisho kwa kuwavaa Majimaji wakiwa kwao Songea.

Kama utakuwa umegundua, mechi zote nne ambazo ni muhimu kwa ubingwa kwa Yanga, zitachezwa ugenini na kama Yanga watafanya mchezo, wanaweza kuteleza.

Yanga imepoteza mechi moja tu dhidi ya Coastal Union na yenyewe ilichezwa ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. Hivyo, ugenini bado si sehemu salama sana kwa Yanga.

Wakati hayo yanaonekana ni vikwazo, uchaguzi mkuu wa Klabu ya Yanga umepangwa kufanyika Juni 5 jijini Dar es Salaam. Jambo ambalo naona kwamba Yanga inaweza kujitafuna na kukosa ubingwa katika hatua za mwisho, hasa kama hawatakuwa makini.

Siku ya uchaguzi ni Juni 5, lakini kawaida uchaguzi unakuwa mrefu na unajumuisha mambo mengi kama kampeni, usajili na mengine mengi ambayo huanza kabla.

Ukiangalia, mechi nne za Yanga zinaanza Mei 5 hadi Mei 21. Hizi ni 16 ambazo zinakwenda haraka na Yanga wanataka utulivu wa hali ya juu, umoja wa nguvu zaidi kuhakikisha wanamalizia mkia wa ng’ombe vizuri.

Utaona, siku hizo hazitakuwa na utulivu kwa kuwa wakati wanasubiri kucheza dhidi ya Stand, Mei 5, siku mbili kabla ambayo ni Mei 3, watakuwa wameanza mchakato wa uchaguzi.

Kwa hiyo, mechi zote nne ambazo mwisho wake ni Mei 21, Yanga watazicheza wakiwa ndani ya michakato ya uchaguzi huo wa viongozi. Hakuna asiyejua kuhusiana na uchaguzi unavyokuwa na ndiyo kipindi cha makundi na mgawanyiko. Kipindi ambacho Yanga mmoja anaweza kumuona mwingine adui, mmoja aliye tayari kumpoteza mwingine na kadhalika.

Mei 4 hadi 9 wagombea watachukua fomu na kurudisha, Mei 10 ni kamati ya TFF kufanya mchujo. Utaona, hapa pia kuna  watu watakatwa, hawatapenda na mvurugano utaibuka, hata uwe wa chinichini, hasa baada ya majina kubandikwa Mei 11.

Mei 12 na 13, kitakuwa ni kipindi cha kupokea na kuweka pingamizi kwa wagombea wote na siku mbili zitakazofuata TFF itapokea na kupitia pingamizi zote na kufanya usajili wa wagombea. Mei 16 majina baada ya usaili, yatatangazwa.

Mchakato utaendelea na Mei 20, siku moja kabla ya Yanga kumaliza mchezo wa mwisho wa ligi, Kamati ya Maadili ya TFF itatangaza maamuzi ya kamati na Mei 21, siku Yanga inacheza mechi ya mwisho ya ligi, kitakuwa ni kipindi cha kukata rufaa kwa maamuzi ya masuala ya kimaadili kwenye Kamati ya Rufaa ya Maadili TFF.

Hiki ndicho nilikuwa ninalenga, kwamba wakati wa michakato yote hii, kweli Yanga wanaweza kuwa watulivu, wakayashinda makundi ya uchaguzi na kupigana kwa umoja kubeba ubingwa?

Hakuna anayeweza kukataa, uongozi unaweza kuhujumiwa usitwae ubingwa. Kwa kuwa wapinzani wangependa kuona unafeli, ili waupinge kwenye kampeni, kuliko ukibeba ubingwa wa ligi na Kombe la FA, utakuwa umejipigia kampeni.

Uongozi pia, hauwezi kufanya kazi zake kwa uhakika. Utakuwa kwenye kampeni na mapambano ya mechi zilizobaki mkono wa kulia, huku ikishambulia na mkono wa kushoto kwa kupambana na kampeni!


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic