Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ameambiwa kuwa kosa kubwa ambalo alilifanya katika miaka ya hivi karibuni ni kutomsajili mshambuliaji Luis Suarez.
Julai 2013, Arsenal ilikuwa na nafasi ya kumsajili mshambuliaji huyo aliyekuwa Liverpool, ambapo Arsenal ilikuwa tayari kutoa pauni milioni 40, Liverpool ikasema kuwa ipo tayari kumuuza lakini ikawataka Arsenal waongeze mkwanja ili wampate.
Kichekesho ni kuwa Wenger alisema klabu yake ipo tayari kuongeza pauni 1 tu katika dau hilo, majibu hayo yalionekana kama dharau kwa Liverpool ambayo ikigoma kumuuza na baadaye mwaka 2014 ikamuuza mchezaji huyo kwenda Barcelona kwa pauni milioni 65.
Kauli hiyo imetolewa na beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher ambaye alicheza pamoja na Suarez kikosini hapo.
“Wenger amekuwa makini sana katika masuala ya fedha, huwa hana haraka katika masuala ya kutumia fedha lakini kuna muda inabidi awe makini na matumizi yake ya fedha.
“Naamini kama wangekubali kutoa pauni milioni 50, wangeweza kutwaa hata ubingwa wa Premier League mara mbili ndani ya miwimi mitatu. Suarez ni muhimu sana kikosini, jinsi anavyocheza ni kwa kiwango cha juu,” alisema Carragher.
Mara baada ya kutua Barcelona, Suarez amekuwa na msaada mkubwa kikosini hapo na kutwaa mataji mengi ambayo ni La Liga (2014/15), Copa del Rey (2014/15), UEFA Champions League (2014/15), UEFA Super Cup (2015) na FIFA Club World Cup (2015).
0 COMMENTS:
Post a Comment