April 18, 2016

Ngoma (kulia) akiwa na Pato Ngonyani.

Na Saleh Ally
UKIZUNGUMZIA wachezaji hatari wanaosumbua kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, basi itakuchukua muda mrefu sana kuwataja wanaotokea hapa nyumbani.


Ukianzia kwa wafungaji, lazima utasema Hamisi Kiiza wa Simba anaongoza, huyu ni Mganda. Anafuatiwa na Mrundi, Amissi Tambwe halafu Mzimbabwe Donald Ngoma, hawa wote wa Yanga.


Kama utataka kuzungumzia mshambuliaji hatari kabisa ambaye anaonekana kuwa msumbufu na mwiba kwa mabeki wa timu pinzani, kamwe hutaacha kumtaja Ngoma tena. Lakini Kipre Tchetche wa Azam ni kati ya wanaoingia katikati, yeye amekuwa akitamba karibu kila msimu, huyu ni raia wa Ivory Coast.


Huu ni msimu wa 2015-16, ambao tayari wanaowania ubingwa wameishajitenga. Yanga, Simba na Azam FC.


Msimu uliopita, mshambuliaji hatari zaidi na aliyekuwa anatikisa alikuwa ni Emmanuel Okwi wa Simba, huyo ni Mganda, pia aliwahi kuichezea Yanga na akaifunga Simba. Tangu ameondoka yeye, Simba inaonekana kupwaya si kidogo.


Watanzania wapo, mfano Simon Msuva wa Yanga, Ibrahim Ajib wa Simba, John Bocco wa Azam FC na wengine ambao utaona kiwango chao kimekuwa kikiendelea kubaki katika nafasi ya saizi ya kati.


Kuna sababu ya kujipima katika hili ili kuona kama tunakwenda sawasawa au tuko palepale na tumekuwa tukijisifia katika kitu ambacho hakina msaada na mpira wa Tanzania.


Kwanza sina maana kwamba wachezaji wa kigeni wasitambe au kufanya vizuri. Itakuwa bora zaidi ikiwa hivyo ili wawe changamoto kwa wale wazawa. Lakini vipi wazawa hawaonyeshi kuwa changamoto kwa wageni?
Mfano sasa wangekuwa wanashinda kwa karibu angalau Kiiza na Msuva au Tambwe na Ajib. Lakini ni Kiiza dhidi ya Tambwe na hakuna dalili ya mfungaji bora kutoka hapa nyumbani.


Bado ninaona tunaweza kujipima, kwamba kweli Ngoma na wenzake wana kiwango cha juu sana au washambuliaji wengi kutoka Tanzania wana viwango vya kawaida ndiyo maana wageni wanaonekana kuwa na kiwango cha juu sana? Lazima tuliangalie hilo.


Lakini kama hilo halitoshi, bado kuna kila sababu ya kuangalia hili, kama wachezaji wa Tanzania wanashindwa kuwa katika kiwango cha juu muda wote, tatizo ni wao au uongozi wa timu wanazozitumikia?
Nasema uongozi wa timu kwa sababu hii; huenda wageni wamekuwa na malipo makubwa sana hadi mara tatu au nne dhidi ya wazawa. Wanalipiwa nyumba na kupewa usafiri wa hadhi ya juu, au familia zao zinapewa huduma nyeti kama matibabu na wazawa hawapati hata nusu ya hilo, hili litakuwa ni tatizo la uongozi.


Watu wote kulipwa wakalingana, haiwezekani. Lakini kuna mambo muhimu kama huduma ya afya, makazi na nyinginezo huwa zinalingana kwa kuwa wachezaji ni binadamu na wangependa kutimiziwa mambo muhimu. Hilo liangaliwe na ikiwezekana kuwapa matumaini na kuonyesha kuwaamini wachezaji wazawa, nayo itasaidia.

Tambwe

Kwa upande wa wachezaji, wao pia wanaweza kuwa tatizo kwa kuwa tunaona wanapewa nafasi lakini wanashindwa kufanya vema au wanashindwa kuzitumia nafasi hizo kuonyesha wanastahili.


Kingine ni wale waliofanya vizuri kwa muda mchache tu, wanaporomoka mara moja jambo ambalo huwezi kulitarajia. Mwisho wanaishia kulaumu viongozi wakati chanzo ni uzembe wao unaotokana na kuvimba kichwa au kuona hakuna kama wao baada ya mafanikio kidogo kabisa.


Kingine ni suala la kujituma zaidi na kuwa na ndoto. Inawezekana viongozi wanaweza kuwa sehemu ya kuwakatisha tamaa. Licha ya hivyo, lakini wazawa wana kila sababu ya kuzimaliza hisia za wageni ndiyo bora zaidi kwa kucheza soka la uhakika na kuwa msaada kwenye timu.


Hawapaswi kulimaliza hilo kwa kuwachukia, kusambaza majungu na maneno ya chini au kuwanunia na kuwanyima ushirikiano, badala yake ni ushindani ulio wa haki kwa lengo la kuisaidia timu lakini kupandisha uwezo binafsi na kujitengenezea soka bora ndani na baadaye kimataifa. 

Okwi

Waungwana lazima mbadilike, tuachane na hadithi za kuamini Tanzania ina vipaji sana wakati mafanikio ni duni. Kila mmoja ajipime aone anakwama wapi ili afanye marekebisho. Hebu mtafakari hili halafu wakati mwingine nitalianzisha tena.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic