April 18, 2016

HASSAN Kessy amesema hataitumikia tena Simba kufuatia mchezaji mwenzake, Muivory Coast, Vincent Angban kumchapa ngumi baada ya kipigo kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara katika Uwanja wa Taifa, Dar, jana Jumapili.

Angban alimvaa Kessy na kumtandika ngumi akimtuhumu kutumiwa na Yanga kuihujumu Simba kufuatia kupewa kadi nyekundu dakika ya 47 baada ya kumchezea vibaya Edward Christopher wa Toto.


Baada ya mchezo huo, Angban ambaye alidaka kwenye mchezo huo, alimfuata Kessy na kuanza kumshambulia kwa ngumi akimtuhumu kutumiwa. Kinachomuumiza Kessy ni kwamba hakuna aliyemtetea na viongozi wote walionekana kusapoti kitendo alichofanyiwa na raia huyo wa Ivory Coast.

“Sitaki kuichezea tena Simba, mkataba wangu unaisha baada ya msimu huu na sitaongeza tena, siendi tena mazoezini, haiwezekani mimi nionekane ninaihujumu timu.

“Tangu nilipofanya makosa dhidi ya Yanga, nimekuwa nikisakamwa na kutafutiwa visa ili nionekane mbaya, kwa hiyo wacha mimi niondoke, watafute beki mwingine wanayeona anafaa,” alisema Kessy.

Alipotoka vyumbani, Kessy alikutana na kundi kubwa la mashabiki wa Simba waliokuwa wakimpigia kelele na kumtuhumu kutumiwa na Yanga, hali ambayo ilizidi kumchanganya na kutamka kuwa hataki kuichezea tena timu hiyo.

Kessy aliingia kwenye mgogoro na Simba baada ya kufanya makosa yaliyosababisha bao la kwanza la Yanga lililofungwa na Donald Ngoma.

Katika hatua nyingine, baada ya mchezo huo wa jana ambao Simba ilifungwa 1-0, uongozi uliwazuia wachezaji wa Simba kupanda basi la timu, badala yake kila mchezaji alipewa nauli ya Sh 10,000 apande usafiri anaoujua lakini basi likarudi tupu. Hakuna kiongozi yeyote wa Simba aliyepatikana kulitolea ufafanuzi hilo.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe, alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya mashabiki kumzonga jana baada ya mechi wakimpigia kelele wakidai hawamtaki Makamu wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’. 

2 COMMENTS:

 1. kwa style hii Simba SC nitaifananisha na timu za Ndondo Cup, sasa unampa mchezaji shilingi elfu kumi kama nauli unategemea anafikaje huko anakokwenda na ajabu basi linarudi tupu kwanini sasa wanafanya hivi?

  kwa hali hivyo ilivyo huku matokeo mabaya yakiendelea wanadhani kwenye mbio ya kusaka ubingwa, timu itaweza kuongeza bidii?

  ReplyDelete
  Replies
  1. Ukweli inasikitisha sana jamani,simba kama faru dume!Ngumi hadharani sasa unategemea ikashiriki mashindano ya kimataifa kweli?

   Delete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV