MARTIN CHACHA, ALIYEKUWA MKURUGENZI WA MASHINDANO TFF, AMEACHIA NGAZI AKIELEZA SABABU NI FAMILIA! |
Na Saleh Ally
TUMEZISIKIA sauti za baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakisikika wakipanga matokeo na wanaomba rushwa tena kwa umahiri mkubwa kabisa.
Tunawajua ni akina nani na haiihitaji mjadala hata kidogo lakini ili kufuata utaratibu, tumeamua kusubiri vyombo husika vilifanyie kazi hili jambo.
Wakati vyombo husika vikiendelea kufanya kazi kamwe hatuwezi kufumba midomo na kuyaacha yaliyotokea yasahaulike wakati tunaujua ukweli.
Najua, wapo wahusika ambao wangeweza kuzungumza na kuchangia katika hili kwamba kilichotokea ni kitu kibaya kabisa katika maendeleo ya mpira wetu.
Najua, wapo wanaotamani kusema lakini ni waoga, wanaogopa kuumizwa. Najua wapo wanaotamani kuzungumza na kuweka mambo hadharani, lakini wamebanwa na uswahiba au mioyo midogo inayonunulika kwa maneno ya kuvutia au vinginevyo.
Lakini wapo wachache walio tayari kusema. Najua, kwa sasa ukweli utageuzwa na kuitwa chuki, ‘umetumwa’ au ‘unatumiwa’ lakini waliofanya upuuzi huo mkubwa wa karne tangu mpira uanzwe kuchezwa Tanzania watasahau kuwa wao ndiyo walioanzisha.
Mimi naijua sauti ya aliyekuwa akipanga rushwa, naijua sauti ya aliyesema amepewa kazi ya rais, lakini najua hata viongozi wa Geita Sports waliokuwa wakizungumza ni akina nani.
Ajabu na kinachoniumiza kabisa, ni kusikia wahusika wakilalamika eti wameonewa. Wanalalamika eti wametengenezewa sauti, hili ni jambo baya na linaloumiza mioyo ya wapenda soka na wanaotamani kuona mpira wa Tanzania unaendelea.
Watu wajinga, wenye tamaa ya kuona wanafanikiwa binafsi badala ya maendeleo ya nchi yetu katika soka, leo wanaona wanaonewa wakati wameishi wakiuonea mpira na Watanzania wote kwa muda mwingi.
TFF imekuwa ni kijiwe cha maswahiba, watu wanaotaka kukaa na kuifanya kama ya familia. Sasa wamechafua kwa mkono wa kulia na wanataka kufuta na mkono wa kushoto.
Ninawapa taarifa mapema, huu ni wakati mwingine, ni kipindi ambacho Watanzania wanataka haki, hili litafikia mwisho ambao haki itachukua mkondo wake na ukweli utajulikana.
Niwakumbushe wadau wa soka mliokuwa mkilalamika kuhusu maendeleo ya soka lakini leo mmekaa kimya. Adui mliokuwa mkiwatafuta, wamepatikana na mmewajua, semeni na muombe sheria ichukue mkondo.
Ajabu kabisa kusikia waliotenda, wanajua wametenda, wanajua ni wao, wanajua walikuwa na nia mbaya kwa mpira wa Tanzania lakini wameendelea kulalamika muda wote eti wameonewa.
Wameshindwa kuwa na huruma kwa mpira wa Tanzania, lakini wananishangaza wameshindwa kuona hata haya kibindamu. Ninajua hawa watu wana mioyo kweli, lakini vipi mioyo hiyo haijui maumivu ya wengine?
Najua, kuna makundi leo yanakaa kutafuta namna ya kuwavunja nguvu wanaopambana katika hili ili sheria ichukue mkondo wake. Wako wenye nguvu ya fedha ambao wanataka kuwaokoa ‘wabaya’ wa mpira wa Tanzania.
Ninaamini wana uwezo wa kuchelewesha tu, lakini mwisho haki itapatikana na wazandiki waliokuwa wakitudanganya, watakutana na mkono wa sheria.
Tulisikia tuhuma za waamuzi kuhusiana na rushwa, tuhuma za rushwa kuwahusu wachezaji lakini leo hii, tuhuma za rushwa zipo makao makuu ya soka nchini.
Mungu atusaidie, atupe uvumilivu kwa kuwa sisi wenyewe, tumeamua kuila miili yetu bila ya kujali inavuja damu na uchungu unaotokana na maumivu ya kujiuma.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi, najua amekuwa mgumu kujiuzulu akiamini huenda hili litaisha vizuri. Mimi nabaki palepale, naendelea kumshauri hana sababu ya kuchelewa na huu ni wakati mwafaka, aende tu na kama ana programu nzuri ambazo alifanya, basi hongera sana.
Watanzania wenye akili na uwezo mkubwa wapo wengi, wataendeleza tena huenda kwa uwezo wa juu zaidi.
Nisisitize tena, TFF imechafuka, hili halikwepeki na kuendelea kubaki ni kujichafua zaidi. Vizuri Malinzi akatumia busara, akajitazama tena na kuondoka kwa kuwa akifanya hivyo, itasaidia kuacha nafasi nzuri kwa uchunguzi na kama bado heshima yake ipo juu, atailinda kuliko kuendelea kubaki na kuichafua.
SOURCE: CHAMPIONI
SOURCE: CHAMPIONI
HII NI VITA KALI KATI YA RUSHWA V/S MAADILI YA UONGOZI WA SOKA TANZANIA.IWAPO WATUHUMIWA WATAONEKANA HAWANA HATIA BASI RUSHWA ITAKUWA IMESHINDA KWA KISHINDO NA HUO UTAKUWA MWISHO WA MAADILI YA SOKA TANZANIA NA TUTARUDI NYUMA MIAKA KUMI ILYOPITA ENZI ZA FAT
ReplyDeleteUchunguzi wa TAKUKURU unapaswa kuanzia kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kama kuna rushwa ilipita huko wakati wa kujadili kashfa hii na kwa nini watuhumkiwa wengine waliachwa na wengine hawakuitwa kabisa mbele ya kamati hiyo
ReplyDelete