April 9, 2016


Na Saleh Ally
SIKU iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi wa soka, imewadia. Siku ambayo mabingwa wa soka Tanzania, Yanga wanashuka dimbani kucheza na Al Ahly ya Misri katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Al Ahly ni vigogo na timu kubwa mara nyingi kuliko Yanga, hii ni katika historia ya soka Afrika. Ukizungumzia Tanzania, Yanga inabeba mengi kuliko Al Ahly.

Mkubwa na mkubwa kwa maana ya historia, lakini si rahisi kupinga ukubwa wa rekodi za Waarabu hao wa Afrika Kaskazini ambao wameutawala mpira wa bara hili kwa kipindi kirefu.

Soka linabadilika, Simba waliing’oa Zamalek ya Misri ikiwa bingwa Afrika na timu bora Afrika. Al Ahly ya sasa ni ngumu kuliko ile ya mwaka 2013, lakini Yanga wakiamua, wakaungana na kupamba vilivyo, watawang’oa.


Al Ahly hawashindi au kufanya vizuri kwa kuwa ni malaika lakini kila kitu kinajengwa kwa misingi na uhakika.

Wanajua huu ni mchezo wa ugenini, basi mipango ya ugenini inachukua nafasi na haya utayaona leo katika mechi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

I: KUMILIKI SANA
Al Ahly wanakwenda na mfumo wa kisasa kiuchezaji unaosema, ‘take the ball to defend the goal posts’.

Msisitizo hapa ni hivi; unapomiliki mpira, hakuna anayeweza kukufunga kwa kuwa utakuwa unalilinda lango lako. Watakaa muda mwingi na mpira wakigongeana, Yanga wanatakiwa kuwapa presha waupoteze ili wao wauchukue na kushambulia.

Wakizubaa wakaona kama wanapiga pasi tu, Waarabu watafurahia sare na itakuwa faida kwao.

II: KUZOZANA
Unaweza kuwaona kama majuha, maana kitu kidogo tu, watazozana muda mwingi na kila mmoja anaingia tena kama wamekasirika kweli. Kumbe wanapoteza angalau dakika moja hadi mbili kwa kila tukio, hapo ujue wako katika ulinzi wasifungwe au wapate sare.

III: KUJIANGUSHA
Hii ni asili kabisa, utaona mchezaji wao anamiliki mpira kwa muda mwingi tena akijaribu kuwachambua mabeki, halafu akiguswa kidogo anajiangusha.

Hapa kuna mawili, moja wanajiangusha kupoteza muda, pili wanajiangusha kupata sehemu nzuri ya kupiga mipira ‘iliyokufa’ ambayo wao ni wazuri, Yanga wawe makini sana na hili, ikiwezekana nahodha wa Yanga azungumze na mwamuzi mapema.


IV: KUSHITUKIZA
Wanajua kuwa wanataka sare, lakini hawawezi kuacha kujaribu. Wanakwenda wanaingia, ukiachia wanatupia. Hivyo lazima kucheza nao huku Yanga wakiamini wanacheza dhidi ya watu wanaojua na walio na uwezo mkubwa. Kulinda pia ni muhimu maana kufungwa nyumbani ni majanga.

V: MASHABIKI YANGA KUFUNIKWA
Al Ahly wanatiwa nguvu nyingi na kelele za mashabiki wao. Hawa ni mashabiki wa soka maarufu zaidi Afrika, wanajulikana kwa jina la Ultras Ahlawy ambao wanapenda kujiita ‘We Are Egypt’.

Hawa jamaa wanajua nini maana ya kushangilia, nini wafanye wakati timu yao imezidiwa, nini wafanye wakati imefunga, wapunguze na waongeze nini kwa wakati upi.

Tofauti kubwa sana na mashabiki wa Yanga na wengine wa hapa wa nyumbani ambao wao ni kuimba na kucheza pekee.

Leo utaona, mashabiki wa Yanga watakuwa wengi kwa idadi, wengi kwa vikundi lakini watafunikwa kabisa dhidi ya Ultras Ahlawy ambao wako jijini Dar es Salaam siku ya tano sasa.

Kwa mfumo wa mashabiki wa Yanga, kuwafunika vijana hao wa Ultras ni ndoto, si jambo zuri kwa walio nyumbani.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV