Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm amesema nahodha na beki wake wa kati wa timu yake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ yupo fiti kucheza mechi ya leo dhidi ya Al Ahly ila ni siri yake kuhusu kucheza.
Cannavaro ni kati ya wachezaji wanaohofiwa na Al Ahly lakini ndiyo kwanza anatokea katika majeruhi ya kifundo cha mguu hivyo kuna shaka ya kuche-zeshwa leo.
Machi Mosi, 2014 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Al Ahly, bao hilo likifungwa na Cannavaro dakika ya 82, hivyo timu hiyo inamhofia katika mchezo wa leo.
Yanga na Al Ahly zinacheza mechi ya leo ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa halafu zitarudiana wiki ijayo nchini Misri, timu itakayopita itacheza hatua ya makundi.
Pluijm amesema kuwa, Cannavaro amefanya mazoezi kwa wiki mbili pamoja na timu akitokea kufanya mazoezi ya binafsi ya gym, hivyo haoni sababu ya kutomchezesha.
“Cannavaro yupo fiti na ninaweza kumchezesha, lakini nina wigo mpana wa wachezaji wenye uwezo, hali inayonipa hamasa ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Al Ahly, hivyo kama nisipompanga Cannavaro, basi nitampanga mwingine mwenye uwezo,” alisema Pluijm.
Cannavaro hakushiriki katika mechi nne za Yanga za michuano hiyo pia nyingine kadhaa za Ligi Kuu Bara mwaka huu kutokana na majeraha aliyokuwa nayo. Amekosa mechi mbili dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius na APR ya Rwanda.
0 COMMENTS:
Post a Comment