April 10, 2016


Ndani ya mwezi mmoja, mshambuliaji wa Simba, Hamisi Kiiza ameweka rekodi ya kuingia kwenye mzozo na uongozi wake kuhusiana na suala la nidhamu.

Kiiza ambaye anaongoza kwa kufunga mabao katika kikosi cha Simba pia Ligi Kuu Bara baada ya kupachika mabao 19, jana aliingia katika mzozo na uongozi wa benchi la ufundi baada ya kukaidi agizo la kuvaa sare kama wenzake.

Kiiza alitakiwa kuvaa sare na kutumia basi la Simba, badala yake akatumia gari lake binafsi na kuvaa nguo za kawaida wakati wachezaji wa Simba walipokwenda Uwanja wa Taifa kuangalia Yanga ikiivaa Al Ahly.

Kutokana na uamuzi huo, Meneja wa Simba, Abbas Ally ‘Gazza’ akaamua kumuondoa kambini.

Hata hivyo Kiiza amejitetea kwamba alikuwa na mkutano na mmoja wa viongozi wa kamati ya usajili ya Simba, Kassim Dewji.

Pamoja na hivyo, meneja huyo alishikilia msimamo wake, kwamba Kiiza alipaswa kuomba ruhusa au kutoa taarifa kama ana mkutano, lakini si kukaa kimya halafu anakwenda uwanjani bila sare pia akiwa na gari lake wakati walikubaliana kutotumia magari binafsi wanapokuwa kambini. Sasa Simba ipo kambini Dege Beach.

Hii ni mara ya tatu kwa kuwa kabla Kiiza aliingia kwenye mzozo na uongozi baada ya kumtetea Isihaka Hassan kwamba alionewa licha ya kujua alimjibu kwa kauli ya ukorofi Kocha Jackson Mayanja.

Uongozi wa Simba ukamtaka kukanusha taarifa hizo alizozitupia mtandaoni, ajabu yeye akakurupuka na kusingizia eti magazeti yaliandika wakati Isihaka alisimamishwa jioni na yeye akaandika mtandaoni usiku, hakukuwa na gazeti lililokuwa limeandika.

Wakati hilo halijaisha, ndani ya wiki mbili, Kiiza amechelewa kurejea kambini Simba kwa zaidi ya siku tano wakati akiwa Uganda, uongozi wa Simba umemuandikia barua kumtaka ajieleze.

Wakati hilo pia halijaisha, sasa Kiiza ameingia kwenye mzozo na meneja wa timu hiyo Gazza kwa kutotii walichokuwa wameelezwa wachezaji wote.


2 COMMENTS:

  1. We Saleh huyo KIIZA hautamuweza kamwe,unataka afukuzwe ili yule jamaa yako Serunkuma arudishwe kikosini na hilo sisi viongozi hatutalikubali!

    ReplyDelete
    Replies
    1. Subirini mpaka auze mechi ndio mtashika adabu.

      Delete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV