April 13, 2016Saa chache tu baada ya Simba kufungwa na Coastal Union kwenye robo fainali ya Kombe la FA, kocha wa Wekundu hao, Mganda, Jackson Mayanja ameibuka na kuwataja Hamis Kiiza na Juuko Murshid ndiyo wamewamaliza katika mechi hiyo.

Katika mchezo huo uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar uliisha kwa Simba kupigwa mabao 2-1 na Coastal kukata tiketi ya kuungana na Yanga, Azam na Mwadui FC katika nusu fainali ya kombe hilo.

Mayanja amesema kuchelewa kurejea kutoka timu ya taifa kwa wachezaji hao raia wa Uganda waliokuwa kwenye mipango ya mechi hiyo ndiko kulikochangia kufungwa kwao.

Lakini pia Mayanja akamtaja kiungo Mwinyi Kazimoto aliyekuwa majeruhi kwamba kukosekana kwake kuliondoa muunganiko kutoka eneo la katikati mpaka kwa mastraika wa timu hiyo.

Aidha, ukiachana na Kiiza kuingia kipindi cha pili Mayanja amesema pia alishindwa kumtumia Juuko katika mechi hiyo kutokana na kufanya mazoezi na kikosi kwa siku chache tofauti na wachezaji wengine aliokuwa nao siku zote.

"Wachezaji hawakuwa kwenye kiwango chao kabisa, muunganiko wa timu ndiyo ilikuwa tatizo. Wachezaji kama Juuko na Kiiza hawakuwa mazoezini kwa muda mrefu na walihitajika pia katika mchezo huu lakini nikashindwa kuwatumia sawasawa kutokana na kuwa nje ya programu kwa muda mrefu.

"Kazimoto naye amekuwa akiunganisha timu lakini hakuwepo katika mechi ya Coastal, ikaonekana ni tatizo kutoka katikati kupeleka mashambulizi kwa mastraika. 

Pamoja na yote lakini hata wachezaji wengine walicheza chini ya kiwango, siyo ule uwezo tuliokuwa nao kwenye mechi za mwisho za ligi kwa tulivyopambana na tukafanikiwa kuwa kwenye hali nzuri.

"Sasa kwa kuwa tumeshapoteza huku kwenye FA ambako kulikuwa na nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa inatubidi tupambane zaidi na tuhamishie nguvu zetu kwenye ligi kuu," alisema Mayanja kocha wa zamani wa Coastal na Kagera Sugar.


Pamoja na hayo, Kiiza aliyeingia akitokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Justice Majabvi, ilimchukua dakika nne kufunga bao la kusawazisha matokeo kuwa 1-1 kabla ya dakika ya 85, Yusuf Sabo kuifungia Coastal bao la penalti lilioamua matokeo ya mchezo huo.

SOURCE: CHAMPIONI

2 COMMENTS:

  1. Sasa wewe saleh na wenzako mliokuwa mnashabikia kutimuliwa kwa Kiiza toka kambini mmeona umuhimu wake?Jamaa kaingia tuu na kutupia nyavuni,huyu jamaa anajua sio hao mabishoo wenu akina Ajabu ajabu!

    ReplyDelete
  2. Sasa wakati wa Mayanja kutimuliwa umefika,kassim Dewji amekasirika sana kwa Kiiza kutimuliwa kambini na pia kuwekwa benchi katika mechi ile.Kwa kuona umuhimu wake,Dewji amempa Kiiza gari mpya kabisa ili aendelee kuichezea msimbazi na huyo jackson ndio baibai tena!

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV