April 11, 2016


Katika hali isiyo ya kawaida, juzi Kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa, alijikuta kwenye hali ngumu baada ya kuzungukwa na mashabiki wa Yanga waliokuwa wakimshinikiza kurejea kwenye kikosi chao aje kuwaokoa.

Tukio hilo lilitokea baada ya kumalizika kwa mchezo wa Yanga dhidi ya Al Ahly ya Misri Uwanja wa Taifa, Dar. Mechi iliisha kwa sare ya 1-1.

Wakati Mkwasa akielekea kwenye gari yake ili aondoke uwanjani hapo, ndipo kundi kubwa la mashabiki wa timu hiyo likamzuia asiondoke na kumtaka arejee kikosini mara moja wakidai kuwa tangu ameondoka mambo hayaendi vizuri.

Ingawa Mkwasa alijaribu kuwatuliza mashabiki hao lakini wao waliendelea kung’ang’ania kuwa hakuna mjadala zaidi ya kurudi nyumbani huku wengine wakienda mbali na kumlalamikia kuwa timu haina stamina na haichezi kama yeye alipokuwa msaidizi wa kocha mkuu, Mdachi, Hans Pluijm.

 “Sisi mashabiki wa Yanga, tunakuambia urejee kikosini, tunakuhitaji zaidi huku kuliko timu ya taifa. 

Timu kwa sasa hatuielewi, haina stamina hata mabao mengi tuliyokuwa tukifunga kipindi ulipokuwepo hakuna tena, kwanza TFF kwenyewe hapaeleweki. Rudi nyumbani tu,” alipaza sauti mmoja wa mashabiki aliyekuwepo kwenye kundi hilo.

Baadaye wakakubali kutulia na kumwacha kocha huyo aondoke uwanjani hapo lakini kwa sharti la kulisukuma gari lake taratibu mpaka nje ya uwanja huo ambapo agizo hilo lilitekelezwa.

Mkwasa aliondoka kikosini hapo hivi karibuni baada ya kukabidhiwa mikoba ya kuinoa Stars iliyokuwa mikononi mwa Mholanzi, Mart Nooij.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV