April 16, 2016



Na Saleh Ally
Mjadala kwamba fedha ni chachu kuu ya mafanikio katika mchezo wa soka, unaweza kuwa sahihi. Lakini mjadala wa fedha si kila kitu katika soka, unaweza kuwa sahihi zaidi.

Kuna mifano mingi sana imekuwa ikijitokeza na inaweza kuwa msaada mkubwa katika kubadilisha mambo katika maendeleo ya mchezo wa soka hapa nchini.

Kwamba ili ufanikiwe, hata kama utakuwa na fedha na vipaji, lazima kuwe na mipango madhubuti kwa ajili ya kusonga mbele.

Mfano mzuri tuliona Al Ahly walichokifanya, walihakikisha wanatuma mapema kabisa ambaye alikuja nchini na kufuatilia kila jambo ambalo waliona walihitaji likae sawa.

Lakini unaweza kushangazwa utakapoona mechi ya Taifa Stars dhidi ya Misri siku zilizobaki ni zaidi ya 30, lakini tayari Meneja wa timu ya taifa ya Misri yuko hapa Tanzania.

Hatujui atakaa kwa siku ngapi, lakini hiyo ni sehemu ya kuonyesha wenzetu wako makini kwa kila wanachokifanya.

Misri iliyumba sana kisoka baada ya machafuko ya kisiasa. Klabu kubwa kama Al Ahly na Zamalek zikaingia kwenye wimbo la ukata kutokana na mashabiki kuzuiliwa kuingia uwanjani.

Utaona hata ushiriki wao katika michuano ya Afrika ikazidi kuwa ya kusuasua. Timu ya taifa pia nayo ikaingia kwenye wimbi hilo ikakosa hadi kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika.

Sasa jamaa wamerudi kazini, wanataka kuhakikisha wanafanya kilicho sahihi na kufanikiwa. Wanataka kuona mambo yanakwenda kwenye msitari ndiyo maana wako kazini sasa.

Yanga tayari imetuma mtu jijini Cairo kufanya maandalizi kabla ya mechi yao ya marudiano ya Jumanne ijayo. Ni jambo zuri, wanapaswa kupongezwa lakini bado inapaswa kujifunza zaidi.

Wanapokuja watu wa Al Ahly, lazima kujua wanachokifanya. Kama kwenda isiwe kufuata mkumbo nasi tunatuma watu kama Watanzania. Lakini lazima kuangalia kila kinachokuwa muhimu kutoka kwao kama kujifunza lakini ikiwezekana kuongeza vile vinavyoonekana muhimu kupitia kwetu.

Soka inahitaji maandalizi ya ndani na nje ya uwanja. Soka inahitaji mipango ya muda mrefu na mfupi na lazima tukubali katika mipango kuna suala la uvumilivu.

Haitatokea hata siku moja, watu wakalala tu halafu mambo yakafanikiwa. Lazima kuwe na watu wanaopambana na mapambano lazima yawe ya akili kwa kuwa unaweza kupambana halafu ukaingia kichwakichwa, kila siku utakuwa unachapwa tu.

Niwakumbushe, maandalizi ya nje pekee hayatoshi lazima kuwe na maandalizi ya uwanjani ambayo pia uongozi kwa kushirikiana na benchi la ufundi lazima uhakikishe kila kitu kinakwenda sawa na sahihi.

Maandalizi ya benchi la ufundi ni kimwili kwa maana ya fitnesi, lakini angalia umuhimu wa saikolojia ambao huu unajumuisha pande hizo mbili yaani benchi la ufundi na uongozi.

Ili wanajeshi au wachezaji wawe tayari, lazima kuwa na utayari wa kila kitu na utakuwa bora kama maandalizi yatakuwa ni ya uhakika kwa asilimia mia.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic