May 31, 2016



KIKOSI CHA TAIFA STARS KILICHOTOKA SARE YA BILA KUFUNGANA NA NIGERIA KWENYE UWANJA WA TAIFA, DAR.

Na Saleh Ally
Ukiangalia katika mechi nyingi za Ligi Kuu Bara utaona mashabiki wamekuwa wakipungua kwa kiasi kikubwa kwenye viwanja vya soka.

Inawezekana kabisa wengi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kabla ya kwenda uwanjani kwa kuwa tu mechi zinaonyeshwa kwenye runinga.

Wanaona kuonyeshwa kwenye runinga kunatosha kabisa. Si jambo baya, Azam TV wameleta mwamko mpya na tunapaswa kuwaunga mkono.

Lakini Jumamosi ya Juni 4, kikosi cha Taifa Stars kitashuka uwanjani pale Taifa kucheza na Misri katika mechi muhimu kuwania kucheza Kombe la Mataifa.

Stars ina pointi moja tu baada ya Chad kujitoa. Inahotajika kushinda mechi zake mbili zilizobaki dhidi ya Misri na Nigeria.

Mechi ya Misri ni nyumbani, Nigeria itakuwa ugenini. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ina uwezo wa kufanya vema na huu ndiyo wakati wa kuiunga mkono.

Haitakuwa sahihi kama watu wote watabaki nyumbani na kuacha Stars icheze pekee pale Taifa huku ikiungwa mkono na Kilimanjaro Premium Lager ambao wameonyesha ni wazalendo wa kweli.

Vizuri watu wajitokeze uwanjani kwa wingi Jumamosi ili kukamilisha ule usemi wa shabiki ni muhimu kwa kuwa ni mchezaji namba 12. Stars inahitaji sapoti yetu tena kwa nguvu zote.

Wanaotakiwa kuingia uwanjani ni watu 60,000 tu ambao hawafiki hata robo ya robo ya idadi ya Watanzania wapenda soka.

Wako ambao watapata nafasi ya kuangalia kwenye runinga kwa kuwa wako mbali na Azam TV inaonekana nchi nzima nan chi jirani. Lakini kwa wale wanaoishi katika jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kuonyesha uzalendo.
Kama wachezaji wa Stars wataona kuna umati mkubwa uwanjani ukiwaunga mkono, basi nao watapambana kutoliangusha taifa na kuwaangusha mashabiki waliojitokeza.

Tusiwaache mashabiki wa Misri waingie Uwanja wa Taifa na kuliteka taifa letu kama walivyofanya wakati Al Ahly ilipokuwa nchini kucheza na Yanga.

Hata kwao kuna runinga zinazoonyesha live. Lakini mashabiki hujitokeza kwa wingi kwa kuwa wanajua umuhimu na faida ya kuwa uwanjani kuwachanganya wapinzani na kuwaunga mkono wanajeshi wao wanaopambana kwa ajili ya taifa. Twendeni Taifa tukapambane pamoja na Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic