June 2, 2016

WATANGAZAJI WA KIPINDI CHA SPORTS EXTRA AMBAO NI WAANZILISHI WA NDONDO CUP WAKIONGOZWA NA SHAFFIH DAUDA BAADA YA KUSAINI MKATABA NA AZAM TV WAKIWA NA UONGOZI WA AZAM TV, MKURUGENZI RHYS TORRINGTON NA CHALZ HILARY.

Kampuniya Azam Media kupitia kituo chake cha runinga cha Azam TV, inatarajia kuonyesha ‘live’ mechi zote za michuano ya Sports Extra Ndondo Cup ambayo Jumapili hii inaanza hatua ya 32 Bora.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Azam Media, Rhys Torrington, wakati walipokuwa wakiingia makubaliano na waandaaji wa michuano hiyo, Clouds Media ambapo mkataba huo ni wa zaidi ya shilingi milioni kumi.

“Tumepania kuhakikisha tunaufanya mchezo wa soka hapa nchini unapiga hatua hivyo tumeamua kuonyesha mechi zote za Ndondo Cup kuanzia hatua hii ya 32 Bora ambapo chaneli zetu za Azam Sports HD na Azam Two ndizo zitaonyesha.

“Naomba tuwe pamoja kwa hili ili kuifanya michuano hii kuwa maarufu na kuifunika ile ya Euro 2016 (michuano ya soka barani Ulaya) ambayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni,” alisema Torrington.

Naye mwanzilishi wa michuano hiyo Shafih Dauda, alisema wanashukuru kuingia makubaliano hayo na Azam kwani itatoa fursa kwa watazamaji hata waliopo nje ya Tanzania kuishuhudia.

Aidha, Dauda aliongeza kuwa, Jumapili hii ndiyo hatua hiyo itaanza kwa kupigwa mchezo kati ya mabingwa watetezi, Faru Jeuri dhidi ya Temeke Market kwenye Uwanja wa Bandari, Dar.


Bingwa wa michuano hiyo anatarajiwa kuondoka na kitita cha shilingi milioni kumi, wa pili Sh milioni tano na wa tatu Sh milioni tatu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV