June 8, 2016

Siku moja tu baada ya kutua Yanga, beki Andrew Vicent ‘Dante’ amemtaja mshambuliaji Donald Ngoma kuwa ndiye alikuwa akimsumbua kwelikweli.

Dante amesema Ngoma ni mshambuliaji msumbufu zaidi na aliyempa wakati mgumu zaidi kila walipokutana na Yanga msimu uliopita.

Dante amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mtibwa Sugar aliyokuwa akiichezea.

Dante ameiambia SALEHJEMBE kuwa Ngoma ni mshambuliaji mwenye mambo matatu ambayo wengi hawana.

“Kwanza ana kasi sana, ni mtu ambaye anaendesha kweli mpira tena kwa kasi kubwa. Pili ana nguvu sana jamaa, kumthibiti inabidi ujipange kweli.


“Kingine ambacho ni cha tatu, ni kazi sana kumpokonya Ngoma mpira. Ukilazimisha ujue utamfanyia madhambi,” alisema Dante.


Dante ni kati ya mabeki waliofanya vizuri kwa msimu uliopita hasa katika suala la ukabaji na amekuwa mchezaji wa nne kusajili wa Yanga msimu huu baada ya Hassan Kessy kutoka Simba, Juma Mahadhi aliyekuwa Coastal Union na kipa Beno Kakolanya kutoka Prisons.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV