June 8, 2016


 Na Saleh Ally
MABINGWA wa soka Tanzania, Yanga wamefanikiwa kufanya usajili wao wa nne juzi baada ya kumalizana na kiungo wa Mtibwa Sugar, Andrew Vincent ‘Dante’.

Dante ni kati ya viungo wataratibu nje ya uwanja, mwonekano wake kama anavyosema mwenyewe ni ‘brother man’, lakini anapokuwa uwanjani ni kazikazi hasa, ni jembe hasa.

Tayari Yanga imewasainisha wachezaji wazalendo wanne, ambao ni kutoka Simba, Hassan Kessy, Juma Mahadhi aliyekuwa Coastal Union, kipa kutoka Prisons, Beno Kakolanya na Dante.

Katika mahojiano na SALEHJEMBE muda mchache baada ya kutua Yanga, Dante mwenye umri wa miaka 24 ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili, anasema miaka mingi alipania kutua Yanga kwa kuwa pamoja na mapenzi na kikosi hicho, alijua ni sehemu bora ya kujiendeleza zaidi.

“Niliipenda Yanga mapema sana, lakini unaona kabisa mambo yao yako kwa mpangilio, pia ni sehemu nzuri kama unataka kufanikiwa na kutoka,” anasema.


SALEHJEMBE: Wewe unamudu namba zipi?
Dante: Kwa uhakika ni namba 2, 4, 5 na 6.

SALEHJEMBE:  Naona umeiruka namba tatu, vipi?
Dante: Kidogo inanisumbua kwa kuwa natumia mguu wa kulia kwa wingi zaidi.

SALEHJEMBE:  Nini kilikuvutia zaidi hadi ukaona Yanga ni sahihi, ni maslahi pekee?
Dante: Maslahi ni jambo jema, lakini niliichagua Yanga mapema kwa kuwa naona mambo yao yako katika mpangilio mzuri, kuna nafasi ya kutoka pia.

SALEHJEMBE:  Kutoka kivipi, fafanua kidogo…
Dante: Nataka kucheza Yanga nifanye vizuri na kuonekana, baadaye nitokea na kucheza nje ya Tanzania.

SALEHJEMBE:  Ungependa kucheza wapi kama ni nje ya Tanzania?
Dante: Afrika Kusini, Ufaransa, Hispania na kwingineko. Lengo ni kwenda kimataifa zaidi.

SALEHJEMBE:  Yanga kuna ushindani mkubwa wa namba, naamini si kama Mtibwa Sugar, hilo halijakupa hofu?
Dante: Ili uwe bora zaidi, lazima ushindane na walio bora zaidi. Mimi nataka ushindani bora zaidi.

SALEHJEMBE:  Wewe ni kati ya walinzi wanaopiga sana vichwa, lakini si mrefu sana. Nini hasa huwa unafanya?
Dante:  Kweli ninafanya sana mazoezi ya kuruka viunzi na mengine yanayosaidia niwe na uwezo mkubwa wa kuruka.


SALEHJEMBE:  Kwa msimu uliopita, safu ipi ya ushambulizi ilikusumbua ukiwa Mtibwa na wenzako?
Dante: Safu mbili za ushambuliaji, Yanga na Azam FC. Walikuwa vizuri sana kimpangilio na ukikutana nao kulikuwa na ugumu hasa.

SALEHJEMBE:  Kwa maana ya mshambuliaji mmojammoja, yupi alikuwa sumu kwenu au kwako?
Dante: Ngoma (Donald wa Yanga).

SALEHJEMBE:  Kwa nini?
Dante: Jamaa ni mbishi, ana nguvu, hataki kushindwa. Lakini sifa hizi tatu washambuliaji wengi hawana. Ana kasi, ana nguvu pia anaficha sana mpira na inakuwa kazi kubwa kumpokonya. Ukilazimisha, utamfanyia madhambi.

SALEHJEMBE:  Kuna wachezaji walikuwa nyota kwenye timu zao kama wewe, walipotua Yanga au Simba, wakaonekana wameshindwa kabisa na wengine wanaomba kuondoka. Umejiandaa na hilo?
Dante: Nilikuambia sina hofu na ushindani. Lakini wachezaji tuna tabia ya kushikiana akili au watu kuiga maisha au mambo ya watu, hilo ndiyo tatizo.

SALEHJEMBE:  Unaweza kulifafanua hilo zaidi?
Dante: Ndiyo, mfano unakuta watu wanakunywa sana pombe, wewe hujawahi. Kwa kuwa unaona kufanya hivyo ndiyo maisha ya kistaa, basi na wewe unaanza kunywa, mwisho unapotea. Mimi najitambua.

SALEHJEMBE:  Kwa muonekano wako ni kama ‘brazameni’ flani hivi, michuano ya kimataifa ina ugumu wake, umejiandaa pia?
Dante: (kicheko), Wengi wananichukuliwa hivyo, lakini kazi yangu huwa inawabadilisha mawazo. Mimi ni mtu wa kazi hasa.

SALEHJEMBE:  Kabla ya Yanga, wapi ulipita kufikia ulipo sasa?
Dante: Kuna akademi ya Chang’ombe nilianzia, halafu Etihadi, hawa walinilea kisoka. Baadaye nikacheza Villa Squad kabla ya kujiunga na Kariakoo Lindi ambako Mtibwa waliniona.

SALEHJEMBE:  Kumbe unatokea Dar es Salaam, mimi nilidhani ni kijana tokea Moro?
Dante: Moro ilikuwa kazini, kiasili kwetu ni Rukwa. Lakini kwetu ni Dar es Salaam ambako ninaishi.

SALEHJEMBE:  Nje ya soka unapenda kufanya nini?
Dante: Niwe mkweli, mimi napenda mifugo, nyumbani tunafuga kuku, mbuzi na ng’ombe, huwa nawahudumia nikiwa nyumbani. Pia napenda sana mbwa na ninao wakutosha tu! 


3 COMMENTS:

 1. utajiendeleza wakati utaishia kukaa benchi mwisho wa msimu utaomba kuachwa kama Paul Nonga

  ReplyDelete
  Replies
  1. Ujue kuchanganya akili yako kabla ya tuhuma,Nadir na wengine wako Yanga kitambo sana,mbona hawajaachwa au kusugua benchi na waanaminika mpaka leo?Dogo ana akili sana na ameshajibu mengi vizuri sana.Mchezaji akijituma na kutambua kuwa mpira ndio ajira yake lazima mwalimu atashawishika.

   Delete
 2. 1.YONDANI
  2.NADIR
  3.BOSSOU
  4.NGONYANI
  5.DANTE

  ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV