June 13, 2016


Neno moja tu, ‘tunanyanyasika’ lilizua tafrani ukumbini kwenye Uchaguzi Mkuu wa Yanga juzi Jumamosi, hiyo ni baada ya Mkuu wa kitengo cha habari na mawasialino, Jerry Muro ambaye alikuwa muongozaji katika uchaguzi huo, kulitamka kuelezea uchungu walionao juu ya uwanja wao binafsi.

Kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikieleza kilio chao kwa serikali kukataa kuwapa kibali cha kujenga uwanja wao eneo la Jangwani kwa kile awali kuelezwa si sehemu salama lakini nao wamekuwa na hoja ya kwa nini mradi wa mabasi yaendayo kasi umeruhusiwa kujengwa pande hizo.

Kupitia uchaguzi huo mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi pamoja na wajumbe wakuu wa bodi ya udhamini ya klabu hiyo, Mama Fatma Karume na mwenyekiti Francis Kifukwe, Jerry alisema Yanga imenyanyasika kwa muda mrefu kwa kunyimwa kibali kuanza ujenzi, lakini ghafla alikatishwa na kelele za wanachama ambao hapohapo walivamia jukwaa kuu na kuanza kumwaga hela kama sehemu ya mchango wao.

Ilifika hatua mabaunsa na walinzi waliingilia kati kuzuia ‘msaada’ huo kuendelea kutokana na utitiri wa wanachama waliojazana jukwaani hapo kila mmoja akitaka kutoa ‘alichonacho’ kisha fedha hizo kuzikabidhi kwa viongozi hao wa bodi ya udhamini.


Akizungumzia tukio hilo, DC Mushi alisema hiyo inaonyesha ni jinsi gani watu walivyo na uchungu na klabu yao na kuahidi kulifanyika kazi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV