June 27, 2016


Wakati Yanga ikiendelea na harakati za kujiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, ghafla kumeibuka mtafaruku baina ya nyota wa timu hiyo, Mrundi, Amissi Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinadai kuwa wachezaji hao walivurugana na kufikia hatua ya kushikana na kudondoshana chini wakipambana walipokuwa kwenye mazoezi ya timu hiyo huko nchini Uturuki walipokwenda kuweka kambi.

Chanzo hicho kilikwenda mbali zaidi na kudai kuwa ingawa sababu ya ugomvi wao haikujulikana tatizo nini lakini walionekana wakirushiana maneno kabla ya baadaye kuvaana wakati programu ya mazoezi ya kocha Hans van Der Pluijm raia wa Uholanzi ikiendelea.

Imeelezwa kuwa wakati ugomvi huo ukiendelea na Tambwe akishikwa kwa ajili ya kutulizwa ndipo Ngoma alipopata upenyo na kumpiga Tambwe usoni na kusababisha kumpasua katika paji lake la uso.

"Baada ya hapo ikawa tafrani lakini Tambwe ikabidi atibiwe kwa ajili ya kumtuliza maumivu, baadaye kocha akazungumza nao kwa ajili ya kuwatuliza na baada ya pale ishu ikapoa, lakini mpaka wanarudi Tambwe na Ngoma hawakuwa kwenye mawasiliano mazuri," kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, baada ya tukio hilo, Ofisa Habari wa Yanga Jerry Muro alipozungumza na Waandishi wa Habari, juzi Makao Makuu ya Yanga, Kariakoo jijini Dar, alifafanua kuhusu ishu hiyo akieleza kuwa ulikuwa ni msuguano wa kawaida ambao hutokea popote pale wachezaji wanapokuwa mazoezini.

"Hapana, haukuwa ugomvi, ilikuwa ni suala la kuingiliana wakati wanafanya mazoezi, hutokea popote na hasa kwa timu yenye ushindani kama Yanga maana Ngoma na Tambwe walikuwa wanacheza timu mbili tofauti kwa hiyo kuingiliana vibaya kwa bahati mbaya wakati mnachuana ni kawaida na hakukutokea ugomvi mkubwa.

"Tambwe na Ngoma wote wapo kikosi cha kwanza kwa hiyo huwezi sema eti walikuwa na bifu kwa kugombania namba ndiyo maana wametibuana, hapana, ni suala la mazoezini tu," alisema Muro.

Championi Jumatatu lilifanya jitihada za kuwatafuta wachezaji hao kulitolea ufafanuzi suala hilo lakini Tambwe hakuwa hewani kwa muda mrefu na hata alipopatikana hakupokea simu ya mkononi hata baada ya kupigiwa zaidi ya mara mbili.

Ngoma naye alipotafutwa mara ya kwanza alionekana kuongea na simu nyingine, alipopigiwa tena simu yake iliita bila ya kupokelewa.


Hata hivyo, Tambwe alipotua kwenye Uwanja wa Ndege akitokea Uturuki usiku wa kuamkia jana alionekana akiwa na bandeji amefunga usoni, hali ambayo inaonyesha ukweli wa suala hilo.

SOURCE: CHAMPIONI 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic