Walinzi wawili wa Azam FC, Paschal Wawa na Shomari Kapombe walitarajiwa kutua nchini jana wakiwa na ripoti ya daktari ambayo itawaruhusu angalau kuanza mazoezi mepesi.
Mabeki hao wanatokea Afrika Kusini walikokwenda kufanyiwa uchunguzi wa mwisho wa afya zao.
Kapombe ambaye ni Mchezaji Bora wa Azam wa msimu uliomalizika hivi karibuni, amekuwa nje tangu Machi mwaka huu, akisumbuliwa na tatizo la mfumo wa damu lililoanza kumsumbua baada ya mchezo wa Taifa Stars na Chad, huku Wawa akiwa nje tangu Aprili akisumbuliwa na nyama za paja.
Wawili hao, awali walilazimika kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi lakini bado hali zao hazikutengemaa na kutakiwa kuwa nje kwa wiki kadhaa kabla ya kwenda tena mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba, ameliambia Championi Jumatano kuwa, nyota hao walitarajiwa kutua nchini jana wakitokea Afrika Kusini ambako watalazimika kusubiri ripoti ya uchunguzi wa afya zao ili kuanza kuwapa mazoezi mepesi.
"Watarudi leo (jana) na kikubwa kule siyo kwamba walikwenda kwenye matibabu, bali walikwenda kufanya 'check up' ya mwisho ambayo ingewaruhusu kuanza mazoezi.
“Sasa sisi tunasuburi ripoti ya huko, jinsi itakavyokuja ndivyo tutakavyoipokea, ndiyo itatupa jibu la lini waanze mazoezi ama kama watakuwa bado hawajafikia muda wa kuanza mazoezi pia tutapokea," alisema Kawemba.
0 COMMENTS:
Post a Comment