Na Saleh Ally
HIKI ndicho kile kipindi gumzo zaidi katika mchezo wa soka. Kipindi cha usajili, kila timu inajaribu kujiimarisha ili kuwa na nguvu ya kutosha msimu ujao.
Wakati wa maandalizi kila timu inajiandaa kuwa bingwa, ingawa baada ya kuanza kwa msimu, taratibu mafuta huanza kujitenga na maji.
Kipindi hiki kwa mashabiki ni kile ambacho wangependa kuona timu wanayoiunga mkono ikifanya usajili wa uhakika.
Upande wa viongozi huwa na presha juu kwa kuwa wanataka kufanikisha usajili sahihi ambao ni bora kwao na wangependa kuona wanafanikiwa kuwapata wachezaji bora wanaowahitaji ili kukiimarisha kikosi chao.
Wakati kila upande ukipambana, kuna kundi moja limegeuka kuwa tatizo kubwa katika zoezi hilo la usajili. Hawa ni wale watu wanaojiita mameneja.
Wengi wao naweza kuwabatiza jina mameneja majalala. Yaani watu wanaojulikana kuwa ni mameneja, lakini ukweli wengi wao ni wajanja-wajanja tu na wanaokuwa katika harakati hizo kwa ajili ya harakati za kutunisha matumbo yao.
Kuna mchezaji mmoja siku chache zilizopita, alikuwa amekubaliana na klabu moja asajiliwe kwa kitita cha Sh milioni 20. Siku ya kwenda kuanguka saini, akaibuka na kusema kwamba anataka kupata Sh milioni 40. Klabu hiyo ikaachana naye na kumsajili mwingine.
Siku chache alirejea na kusema alikuwa tayari kusajiliwa kwa kitita cha Sh milioni 20 tena. Lakini alishachelewa na klabu hiyo ilishasaini mchezaji mwingine, akakosa dili.
Baadaye alieleza majuto yake kwa kuwa alilaghaiwa na mtu aliyejidai ni meneja ambaye alimshawishi kuomba fedha nyingi zaidi akiamini kwamba lazima zingepatikana ili mchezaji huyo afaidike zaidi na meneja aondoke na chake.
Mwisho mchezaji huyo amekosa, meneja hana hasara. Hiyo ndiyo hali halisi ilivyo katika matukio mengi kwa kuwa kuna kundi la watu ambalo limejitokeza na linataka kujenga utaratibu wa kufaidika na fedha wanazolipwa wachezaji wakati wa usajili.
Lakini wachezaji wenyewe wanaonekana bado wako usingizini kwa kuwa wanashindwa kuelewa kwamba wananyonywa au wanatumika kuwafaidisha watu wengine na ikiwezekana wao kutopata wanachostahili. Kuwa na meneja ni jambo zuri, lakini vizuri awe ni yule mtu makini anayefanya kazi kweli kwa ajili ya mchezaji husika.
Vizuri meneja akawa na mchezaji katika kipindi chote ili kufuatilia maendeleo yake, kujali kwa kupigania au kushawishi kuhusiana na maslahi yake lakini si kusubiri wakati wa uingizaji fedha, basi ndiyo awe karibu.
Vichwa vya hao mameneja majalala wanaoibuka kipindi cha usajili pekee vinapaswa kukatiliwa mbali. Badala yake wachezaji wawe makini na kujisimamia vizuri.
Lakini inaweza kuwa vizuri zaidi kama watawatafuta mameneja mapema, hata kabla ya kipindi cha usajili na kuanza kufanya nao kazi katika kipindi ambacho wanajijenga ili kujua uwezo wao, msaada na faida ya kuwa nao na si kipindi cha uingizaji fedha pekee, ndiyo wanainua vichwa vyao.
Kwa kawaida, mchezaji ndiye anapaswa kuwa bosi wa meneja. Lakini meneja anapaswa kuwa kiongozi wa mchezaji na msimamizi wa mambo yake mengi nje ya uwanja, mshauri wa mengi uwanjani pia.
Longolongo imekuwa juu na wachezaji wanaendelea kutumika, amkeni sasa. Mlio wababaishaji, imetosha na muwe na imani na hao wachezaji. Mmewatumia sana kujifaidisha, sasa ni kipindi cha kuwapa nafasi ili nao wazidi kukua kimaisha kwa kuwa wamekuwa wakiyapigania kwa muda mrefu kwa kuwa wana ndoto za kukua.
Pia ni vizuri kwa mameneja wachache ambao wamejitokeza na kuwa makini. Basi wanaweza kuongeza idadi ya wachezaji ili kuendelea kuwaelekeza, kuwasaidia kwa lengo la kuwainua. Pamoja na msaada, pia hili litawasaidia wachezaji hao kuingia kwenye mikono ya mameneja majalala.
0 COMMENTS:
Post a Comment