MSEMAJI WA TFF, ALFRED LUCAS |
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa kitendo cha Klabu ya Stand United kwenda kuwashtaki katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ni sawa na kujisumbua kwani mwisho wa siku lazima suala lao lirudishwe kwao.
Uongozi wa Stand umefikia hatua hiyo ya kuwashtaki TFF kutokana na kuibuka kwa kambi mbili zinazotaka kufanya uchaguzi wa viongozi wapya huku shirikisho hilo likidaiwa kushindwa kutoa muongozo wowote unaohusiana na sakata lao.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema kitendo kilichofanywa na timu hiyo, hakiwezi kuwashangaza kwa kuwa lazima watarejea kwao katika kupata muafaka.
“Kiukweli ninavyofahamu ni kwamba Stand ni mwanachama wa TFF na wala siyo Fifa kwa sababu TFF ndio wanachama katika shirikisho hilo, hivyo kitendo cha wao kukimbilia huko siyo tatizo kwetu, maana lazima watataka mrejesho kutoka kwetu.
“Lakini kwa upande mwingine sisi hatujapata barua au taarifa yoyote kutoka kwa Stand ila haitapita muda lazima Fifa watume taarifa yao kwani mwisho wa siku wao ndio watatakiwa waje kwetu kutafuta muafaka,” alisema Lucas.
Stand hivi sasa kuna mgogoro mkubwa, ambapo kuna makundi mawili. Kuna viongozi wale waliowekwa madarakani na wanachama na wale ambao waliwekwa na TFF.
Hivi sasa kuna mchakato wa uchaguzi, ule wa kundi la wanachama ambalo linajiita wenye kampuni utafanyika Juni 24, mwaka huu, wakati kundi jingine lililowekwa madarakani na TFF ambalo wanachama wanaliita wavamizi, limetangaza kufanya uchaguzi wake Juni 26, hivyo haijulikani kina nani wana mamlaka ya kufanya uchaguzi huo na ni uongozi upi utakuwa halali kikatiba.
0 COMMENTS:
Post a Comment