Siku moja baada ya mlinzi wa kati wa Mtibwa Sugar, Andrew Vicent ‘Dante’ kumwaga wino wa miaka miwili Jangwani, Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime ameibuka na kusema kuwa siyo huyo tu wakitaka wabomoe kikosi kizima na Mtibwa itabaki palepale.
Nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars amesema ni kutokana na timu kubwa za Yanga, Simba kuigeuza Mtibwa kama akademi yao, ameamua kuja na falsafa mpya ya usajili dakika za mwisho kabisa mwa dirisha baada ya kujua safu ipi imepungukiwa.
Maxime aliongeza kuwa kuondoka kwa Dante si ajabu wala pengo kikosini kwake kwani ana fursa za kutosha kupata mbadala wake, ikiwemo michuano ya Ndondo Cup inayoendelea katika viwanja mbalimbali jijini Dar kwani naye ‘aliokotwa’ hukohuko alipokuwa daraja la pili kwenye timu ya Kariakoo Lindi ya Mtwara.
“Wao wabomoe tu, wakitaka wachukue wote. Dante siyo pengo kwetu na mbadala wake atapatikana tu mwishoni mwa usajili. Kama yeye miaka miwili tu amefanikiwa kwenye timu kubwa, nini kinashindikana kupata mbadala wake?
“Mwenyewe nilimuokota daraja la pili, nikamtengeneza msimu mmoja tu, akaitwa timu ya taifa (chini ya kocha Mart Nooij), leo anasajiliwa Yanga, sina shaka naamini kina Dante ni wengi sana Tanzania hii, hata kwenye Ndondo Cup naweza kuwapata wengi tu,” anasema Maxime.
0 COMMENTS:
Post a Comment