June 10, 2016


MKUDE
Kiungo wa Simba, Jonas Mkude amezisikia harakati zinazofanywa na uongozi wa timu hiyo katika usajili wa kuimarisha kikosi chao msimu ujao na katika hilo kiungo huyo ametoa ya moyoni kuhusiana na wachezaji wanaowanyatia.

Mkude ameeleza kuwa si lazima kufanyike usajili wa kuigana au kukomoana na timu nyingine, zaidi ni kuangalia wapi kikosi hicho kiliteleza msimu uliopita na kurekebisha makosa katika nyanja zote ikiwemo ndani ya uongozi ili timu isonge na kupata mafanikio msimu ujao.

“Siwezi kuzungumzia sana katika ngazi ya uongozi lakini kila mmoja aliona tulivyoteleza katika dakika za mwisho msimu uliopita, mfano hata kwa sisi wachezaji wapo wanaolaumiwa kuwa hawakuwa na msaada kwa timu.

“Kwa hiyo kwenye usajili huu watu wawe makini katika kutafuta wachezaji wazuri zaidi tutakaoshirikiana nao msimu ujao, hata hao maprofesheno wawe na uwezo kweli waje kuziba nafasi zilizokuwa na mapungufu ili tusonge mbele na si kusajili kwa kuiga au kukomoana na wapinzani,” alisema Mkude.

Tayari Simba ilishaonyesha nia ya kutengeneza kikosi chake kwa kuwawinda wachezaji wa nje na ndani, ikitajwa kuwahitaji Ramadhani Kichuya wa Mtibwa Sugar, Hassan Kabunda na Idd Mobby wa Mwadui FC na wengine wengi waliopo kwenye rada zao.

Upande wa pili pia ikidaiwa kusafisha kikosi hicho kwa kuwaonyesha mlango wa kutokea Mrundi Emery Nimubona, Mkenya Paul Kiongera, Waganda Hamis Kiiza, Juuko Murshid na Brian Majwega ambao wanaondoka kutokana na viwango duni na wengine utovu wa nidhamu.


1 COMMENTS:

  1. Jamani hajj Manara alisema eti Simba lazima ingekuwa bingwa kutokana na kikosi chao kilivyokuwa kizuri,sasa leo mnasema timu yenu ilikuwa dhaifu sasa isajili kuziba ule udhaifu!Duh nimeamini kunde ikishindwa kuzaa husingizia jua!

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV