June 3, 2016



Na Saleh Ally
IBRAHIM Ajib Migomba, wanamuita Cadabra. Jina linalofanana na lile la utani la Zlatan Ibrahimovich, mshambuliaji nyota raia wa Sweden ambaye asili yake ni ile nchi ya Yugoslavia, sasa haipo tena.

Inawezekana mashabiki au watu waliamua kumuita Ajib jina la Cadabra kwa ajili ya kufanana kwa majina yao ya mwanzo, kama ni uchezaji sidhani, lakini hata ile ‘akili’ ya kutaka mafanikio pia  wanatofautiana sana.

Zlatan alizaliwa Rosengard mjini Malmo, Sweden akiishi katika familia ya kimasikini, mama na baba waliotengana. Mama yake aliuza hadi dawa za kulevya.

Zlatan aliwahi hadi kuiba kwenye supermarket jambo ambalo Ajib sidhani kama amewahi kufanya, lakini baadaye aliapa kujikomboa na alikitambua kipaji chake, alifanikiwa kwa kuwa alikuwa amepania kufanikiwa na misimamo yake yenye nidhamu kuu ya kufikia anachotaka. Sasa baada ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, hauwezi kumkwepa Zlatan kwa ubora.

 Ajib, hana hata nusu ya hicho na kama uwezo uwanjani, hana hata robo ya alichonacho Zlatan. Kama anaamini kweli anafikia alipo Cadabra, basi siku si nyingi atapotea kabisa. Ntakuambia kwa nini.

Wakati fulani nimekuwa nikijiuliza, kwamba inawezekana kabisa Ajib anaona alipo, tayari ndiyo mwisho wa ‘dunia’ na hataki kwenda tena mbele.

Historia inaonyesha hivi; mashabiki wa Simba wanapoona timu yao inafanya vibaya huwavamia viongozi wakati wa Yanga, hutembeza bakora kwa wachezaji wazembe au wanaoonyesha kuzembea.

Asili ya Simba ni kuwadekeza wachezaji, hii hufanywa na mashabiki hata viongozi ndiyo maana nidhamu ya kikosi cha Simba iliporomoka sana hadi kufikia kuonekana kama Kocha Jackson Mayanja anagombana na wachezaji, ilikuwa lazima iwe hivyo.


Kiuchezaji Ajib ni mchezaji anayejitahidi, tuache kumvimbisha kichwa na kuwaaminisha watu ni mchezaji wa kiwango cha juu sana. Takwimu zipo, hizi ndiyo zinazoweza kuzungumza. Amefunga mabao tisa kwa msimu mzima na hana zaidi ya pasi tano zilizozaa mabao.

Hii inatosha kwa Ajib kujipima na kujitambua, pia huu ndiyo wakati mzuri kwake kutofautisha umaarufu wa kwenye ndondo na anachotakiwa kufanya ili kupiga hatua kutoka alipo kwa upande wa Simba ya Tanzania na ikiwezekana kucheza nje ya Tanzania.

Simba wanashindwa kuwa wakweli, wanashindwa kunyoosha mkono na kumuonya Ajib huku wakijua alifanya upuuzi wa kupitiliza kwa kutafuta kadi nyekundu na siku iliyofuata akaondoka kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio kienyeji kabisa.

Alikwenda kufanya majaribio ambayo hatujawahi hata kuona picha zake akifanya hayo majaribio. Tulipewa taarifa kwamba amefuzu lakini hadi leo hii hakuna chochote kinachozungumzwa na uongozi wa Simba haujawahi kupewa taarifa yoyote.



Akiwa Afrika Kusini, meneja wake, Juma Ndambile alikiri kwamba Ajib aliumdanganya yeye kwamba amekubaliana na uongozi wa Simba, kumbe haikuwa hivyo. Pia meneja huyo alisema Ajib alimdanganya wakala wake aliye Afrika Kusini kuwa mkataba wake na Simba umeisha nay eye Ndambile akalirekebisha hilo kuwa si sawa.

Utaona huyu ni mchezaji asiyejitambua na kama ataendelea na tabia hizo, ataendelea kubadilisha timu moja baada ya nyingine na mwisho utaona kadiri siku zinakwenda anazidi kuporomoka kutoka Simba, kwenda timu nyingine ndogo kidogo hadi ndogo kabisa kama ambavyo tunawaona wachezaji wengi waliotanguliza nyodo ndani ya Simba kama Haruna Chanongo na sasa wako kwenye mteremko kuelekea kusikojulikana.

Sasa kuna msululu mrefu wa wachezaji wa zamani wa Simba kuomba kurejea Msimbazi tena wakipiga magoti kwamba walikosea na hawakujua kama wanakosea. Walio ndani ya Simba wanaendelea kuongeza mbwembe na kuvimba majipu.

Kama uongozi wa Simba hautatoa adhabu kwa Ajib, ndiyo utakuwa unaendelea ule utamaduni wa Simba kutunza na kuyalea majipu ya wachezaji miaka nenda rudi huku ukilia ndani hakuna nidhamu.

Simba ni timu ya wanachama, sauti ni nyingi na kila mmoja ana yake. Mwingine atalia asamehewe na mwingine atalia anaonewa. Lakini mzazi ili amrekebishe mtoto wake mtukutu lazima awe ni mtu mwenye msimamo anayeweza kusimamia anachoona si sahihi.

Ajib anaweza kufanikiwa kama atakubali bado ni mchezaji mdogo sana anayejaribu kutafuta njia ya kutoka. Na kamwe hawezi kutoka kama hana nidhamu na ndoto sahihi zilizotengenezwa kwa matofali ya kujituma, kuheshimu na kutaka kufanikiwa kwa njia sahihi.


Mnaomdekeza Ajib ndiyo mnaochangia kumporomosha. Mnaomuonea aibu kuwa atakasirika ndiyo mnaomdidimiza. Na mnaomuona ni staa kama Ibrahimovich, ndiyo mnaommaliza kabisa. Kwani kama angekuwa ni kuku, ndiyo anakaribia kuanza kuitwa kifaranga. Kwake safari ni ndefu na kwa mwendo anaokwenda sasa, yatakuwa ni maisha ya kujidanganya yanayotengenezwa na filamu badala ya hali halisi.

1 COMMENTS:

  1. Chuki binafsi inakusumbua wewe Saleh,nenda kawahi masjid usije ukashindwa kutamka aaamiin kwa sababu ya husda zako!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic