June 3, 2016

NONGA

Na Saleh Ally
MSHAMBULIAJI Paul Nonga ambaye miezi kadhaa iliyopita alijiunga na Yanga akitokea Mwadui FC, amepeleka barua ya kutaka kuondoka Yanga.

Nonda anataka kuondoka Yanga hata kabla ya muda wake kwisha kwa kuwa ameona litakuwa ni jambo jema kwake kulinda kipaji chake.

Nonga anataka kulinda kipaji chake kwa kucheza. Akiwa Yanga chini ya Kocha Hans van der Pluijm anaona hana nafasi, hivyo inaweza ikaua kipaji chake.

Nonga anaamua kuondoka kwa kuwa ushindani ni mkubwa sana dhidi ya wachezaji wawili wa kigeni ambao wanaonekana ndiyo chaguo la kwanza la Kocha Pluijm raia wa Uholanzi.

Nonga anataka kwenda sehemu nyingine ambayo atapata nafasi ya kucheza. Tafsiri yake ni hivi, Nonga anataka kwenda sehemu ambako atakutana na wachezaji wenye kiwango cha kawaida na si kama kile cha akina Ngoma aliyefunga mabao 17 au Tambwe aliyepachika mabao 21.

Nonga atafurahi akienda katika timu ambayo washambuliaji wake si wakali sana ilia pate nafasi ya kucheza. Lakini kuendelea kubaki katika sehemu yenye ushindani, anaweza kuua kipaji chake ambacho anaamini huenda kwa sasa kipo juu sana!

Tanzania imekuwa ikilalama kuhusiana na kutokuwa na washambuliaji wakali na hasa ukiangalia hapa nyumbani au wale wanaocheza Ligi Kuu Bara. Kweli, wachezaji wa kigeni ndiyo wamekuwa wakiendelea kutamba.


Huenda wakaendelea kutamba milele kwa kuwa mshambuliaji anayeonekana ana aina ya mshambuliaji kweli kama ilivyo kwa Nonga, anaamua kukimbia ushindani na sasa anataka timu yenye ushindani wa saizi ya kati atakaouweza au wa chini kabisa ili autawale na kupata nafasi ya kumwaga ya kucheza.

Nonga ameona hawezi kucheza mbele ya Tambe raia wa Burundi au Ngoma raia wa Zimbabwe. Wote wawili hao hawatokei Ulaya, ni Waafrika kutoka katika nchi ambazo hata kwa maendeleo ya kawaida, kwa sasa haziwezi kuifikia Tanzania.

Unaweza ukajiuliza, kama Nonga atapata nafasi ya kucheza katika timu nyingine, vipi mbona hajawahi kufunga angalau mabao 19 kuonyesha ni mshambuliaji hatari.

Binafsi sikuwahi kuwa na hofu na Nonga kwamba arafeli Yanga na bado ninaamini hivyo kwa kuwa ana vitu vingi vya mshambuliaji bora. Huenda hofu na ugeni wa Yanga bado unamsumbua. Lakini wakati anaanza kuzoea, yeye anaona inapendeza akiondoka!

Pluijm alimchukua akijua ana kitu, rekodi inaonyesha ni mmoja wa washambuliaji wazuri ambao wakitengenezwa wanaweza kuwa bora zaidi. Hata kama umri unakwenda, lakini huwezi kusema Nonga anakwenda kustaafu soka ndani ya miaka mitatu au minne ijayo.

Sasa vipi anaogopa ushindani kutoka kwa Mrundi na MZimbabwe. Vipi anataka aende sehemu yenye ushindani wa chini ilia pate nafasi ya kucheza?

Lakini haushangazwi kwamba Nonga anaweza vipi kukimbia Yanga baada ya nusu msimu. Kweli hiki ni kipimo sahihi kwamba muda aliokaa Yanga unatosha kumfanya Nonda achukue uamuzi wa kuondoka, au kuna kitu kingine ana hofu nacho na ameona akifanye ni siri kwake?

Binafsi sikufurahishwa baada ya kusikia Nonga anaomba kuondoka Yanga. Hii ni picha kwamba washambuliaji wa Kitanzania bado wataendelea kuwa waoga wa ushindani na mfano mzuri ni Nonga.

Maana kama Nonga aliona Tambwe na Ngoma ni bora kwake, huenda lilikuwa jambo jema na bahati kwake kuendelea kujifunza mambo kadhaa akiwa karibu nao. Lakini Yanga itashiriki michuano ya kimataifa ambayo ingeweza kumsaidia kumjenga zaidi.

Lakini anaona ni bora kucheza Stand United, Mwadui FC au arudi Mbeya City tena kwa kuwa ushindani umemzidi? Hii si sawa na inaonyesha kiasi gani Tanzania ilivyo na safari ndefu ya kuwa na washambuliaji bora walio tayari kwa ushindani na kufanikiwa.

Mbwana Samatta, hakuogopa kwenda TP Mazembe, kumbuka timu  hiyo ilikuwa na washambuliaji watano akiwemo Given Singuruma kutoka Zambia ambaye alikuwa hatari wakati huo. Lakini Samatta akajiamini na mwisho akawa staa hata kuliko gwiji wa timu hiyo Tresor Mputu.


Nonga anakimbia nini? Tanzania itafika wapi kama washambuliaji wake ni waoga wa ushindani kama Nonga? Kama kweli Nonga ataondoka Yanga, basi tuendelee kusubiri kutegemea wageni na itafikia hadi timu ya taifa, tutalazimika siku moja kuwabadili uraia akina Ngoma.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic