June 11, 2016

MOHAMED HUSSEIN ZIMBWE...

Na Saleh Ally
WENGI sana walikuwa wakimjua kwa jina la Mohamed Hussein maarufu kama Tshabalala. Lakini sasa anapenda kutumia jina la Zimbwe.

Zimbwe ni jina la babu yake mzaa mama, kati ya wajomba zake waliowahi kucheza soka ni beki Said Zimbwe Mwaibambe aliyewahi kukipiga Yanga. Sasa beki huyo kinda wa Simba, anasema anataka kuendelea kulitangaza jina hilo la familia.

Anasema, umefika wakati mwafaka wa kuachana na jina lake la utani la Tshabalala ambalo linamilikiwa na kiungo nyota wa Kaizer Chiefs na Afrika Kusini, Siphiwe Tshabalala.
Katika mahojiano maalum na SALEHJEMBE nyumbani kwake Magomeni Kagera jijini Dar es Salaam, Zimbwe anasema msimu ujao ndiyo rasmi ataanza kulitumia jina hilo hadi kwenye jezi.

Beki huyo wa kushoto ambaye alichipukia kisoka pia katika timu ya Friends Rangers ya Magomeni Kagera amekuwa na msimu mzuri na wenye mafanikio msimu wa 2015/16 uliomalizika hivi karibuni na suala la nidhamu limekuwa gumzo na kuonyesha ni mchezaji tofauti.

SALEHJEMBE: Kipi kilikufanya ulibadili jina hilo?
Zimbwe: Kuna watu walinishauri mara kadhaa, pia nikaona ni sahihi.

SALEHJEMBE: Lile la Tshabalala ulilipataje?
Zimbwe: Nampenda Tshabalala, wakati nacheza Boom Boom, nilikuwa nina jezi ya Brazil. Basi mgongoni nikaandika Tshabalala, basi kuanzia hapo watu wakanizoea kwa jina hilo.

SALEHJEMBE: Ulipitia Azam FC ambayo inakuza vijana, vipi ukaona Simba kunafaa zaidi?
Zimbwe: Kweli Azam FC wanajitahidi, nilikaa kwa misimu mitatu hivi. Lakini baada ya ujio wa Stewart Hall nikaamua kuondoka.

SALEHJEMBE: Hukufurahishwa na Hall, kwa nini?
Zimbwe: Alipofika akasema asingependa kutoa nafasi kwa vijana, labda misimu mitatu ijayo. Hii iliniuma sana, nikampigia simu meneja wangu Herry Mzozo, naye akanishauri kuondoka. Nikabeba begi na kuondoka zangu.


SALEHJEMBE: Ulipataje nafasi Kagera Sugar?
Zimbwe: Mzozo alifanya mazungumzo na Kocha Kibadeni (Abdallah) ambaye alinipa nafasi ya majaribio. Mwisho wakaniambia twende Bukoba na baadaye wakanisajili. Lakini sikuwa na bahati na Kagera hasa mwanzoni.

SALEHJEMBE:Soka ni juhudi, bahati kivipi?
Zimbwe: Mwanzoni nilipofika tu nikaitwa timu ya taifa ‘under 20’, baada ya kurejea Bukoba nikaumia na kukaa nje nusu msimu.

SALEHJEMBE: Baada ya kupona, Kibadeni alikuamini na kukupa nafasi maana ndiye alivutiwa nawe akakusajili?
Zimbwe: Bahati mbaya wakati napona, Kibadeni alishaondoka na Jackson Mayanja alikuwa amechukua nafasi. Yeye naye hakuniamini hata kidogo, yakawa yaleyale.


SALEHJEMBE: Ulimshawishi vipi abadili uamuzi?
Zimbwe: Wachezaji wakongwe kama Nesta na Paul Ngwai walimuomba aniamini. Alianza kunipanga mechi dhidi ya Ashanti, baada ya hapo akaniamini mechi nane za mwisho nikacheza zote.

SALEHJEMBE: Nilisikia ulitaka kwenda Ulaya kabla hata ya kujiunga Simba, ilikuwaje?
Zimbwe: Nilifanya vizuri katika mechi hizo, ikiwemo ile krosi iliyozaa bao dhidi ya Simba. Sasa baba yangu mdogo anayeishi Uholanzi akanishauri kusajili timu itakayokubali mkataba wa mwaka mmoja tu ili baadaye niende kufanya majaribio Ulaya, nikakubali.

SALEHJEMBE: Vipi sasa ulisaini Simba zaidi ya mwaka mmoja?
Zimbwe: Kuliibuka mkanganyiko, meneja Mzozo alitaka nisaini Simba ambao ingekuwa zaidi ya mwaka mmoja. Kagera walikubali nisaini mwaka mmoja kama ambavyo baba yangu mzazi alivyotaka pia.


SALEHJEMBE: Ndiyo, sasa vipi ulisaini Simba?
Zimbwe: Meneja wa Kagera, Mohammed Hussein alituchukua mimi na wachezaji wengine kwenda Bukoba kwa ajili ya kusaini mikataba. Niliamua kuondoka bila ya kumuaga Mzozo ili kutimiza ndoto yangu ya kucheza UIaya. Nikiwa njiani eneo la Chalinze nikawa natumiwa meseji na watu wananiambia mambo hayakuwa mazuri nilipoondoka na Mzozo alichukia sana.
Ingawa nilitaka niwafuate wazazi wangu na kusaini Kagera, lakini niliona ninamuangusha Mzozo ambaye alinisimamia tangu nikiwa mtoto katika masuala ya soka.


SALEHJEMBE: Ukaamua kuchukua uamuzi upi?
Zimbwe: Nikazungumza na baba, naye akaniambia niamue ninachoona sahihi. Nilipofika Morogoro nikamdanganya meneja wa Kagera kuwa nyumbani kuna tatizo. Nikashuka, akanipa nauli nikarejea Dar es Salaam na kuungana na Mzozo, siku iliyofuata nikasaini Simba.

SALEHJEMBE: Vipi kuhusu baba yako mzazi na mdogo wake wa Uholanzi?
Zimbwe: Wote waliniunga mkono, ule mpango bado upo na nina imani, Simba hawana tatizo na maendeleo ya wachezaji wao.

SALEHJEMBE: Uliamua kujiunga na Simba, hukuhofia ushindani wa namba?
Zimbwe: Hofu ilikuwepo, maana Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ nilimjua vizuri, yeye alikuwa timu ya taifa ‘under 20’ mimi tegemeo ‘under 17’. Tena siku chache akasajiliwa Banda, nikajua kazi ipo, lakini niliahidi kupambana kwa juhudi hadi nifanikiwe.


Championi: Mshambuliaji yupi anakupa presha sana unapojua unakutana naye?
Zimbwe: Msuva, huyu nimecheza naye timu ya vijana ya Azam FC na pia timu ya taifa ya vijana, namjua na tunajuana kikazi. Huwa ninajiandaa sana kwa kuwa ana kasi, nashukuru huwa ninamdhibiti vizuri.

SALEHJEMBE: Msimu ulioisha umetoa pasi ngapi za mabao?
Zimbwe: Saba, nyingi nimempa nafikiri Ajib (Ibrahim).

SALEHJEMBE:Una sifa ya mtu mwenye nidhamu, nini kinakufanya uliweze hilo linalowashinda wengi?
Zimbwe: Naamini ni malezi mazuri yaliyofuata misingi ya dini yangu ya Kiislamu.

SALEHJEMBE: Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Hans Poppe ametangaza kukupa gari, vipi umeshakabidhiwa?
Zimbwe: Nilisikia hilo, lakini bado sijakabidhiwa. Nafikiri muda bado.

SALEHJEMBE: Nini kinakusumbua dhidi ya mafowadi watukutu?
Zimbwe: Wako wana maneno machafu, wajeuri lakini najua wanataka kunitoa mchezoni, mara nyingi nakuwa mtulivu, nafanya kazi yangu.

SALEHJEMBE: Timu ya taifa, inaonekana sasa namba tatu unaimudu zaidi lakini kama Kocha Mkwasa (Boniface)  hakuamini, unafikiri kwa nini?
Zimbwe: Wanaochaguliwa kwenye timu ya taifa ni wale waliofanya vizuri kwenye timu zao. Naamini kila mmoja anayecheza anakuwa bora na suala la kupanda namwachia kocha.


SALEHJEMBE: Ni shabiki wa timu gani Ulaya, pia ungependa kucheza wapi nje ya Tanzania?

Zimbwe: Manchester United ndiyo chama langu. Nikitoka nje naweza kuanza Afrika Kusini na kama Ulaya, sehemu yoyote ambayo nitapata timu bora.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV