RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI |
Na Saleh Ally
GUMZO la maendeleo ya soka nchini ndilo kubwa zaidi, lakini bado hakuna mabadiliko makubwa katika michezo na wadau wenye uchungu wameendelea kupambana.
Nani ataendeleza mpira wa Tanzania? Yupi ni mhusika mkuu na anayetakiwa kuwa na uchungu? Mpira wa Tanzania unatakiwa kuendelea huku ukiwa umegubikwa na majungu, chuki, wizi, ubabaishaji na rushwa ya waziwazi lakini kila kitu kinaonekana ni kawaida?
Mpira wa Tanzania unapaswa kuendelea huku serikali ikiwa imetoa mikono yake katika michezo kabisa huku ikijua ni soka la ridhaa ambayo inategemea msaada wake mkubwa?
Viongozi wa serikali, zaidi wanasubiri kukutana na washindi au waliofanikiwa baada ya kupitia njia zao wenyewe zenye ugumu, wao watahusika na kufanikisha hafla na kutoa maneno ya nasaha katika kipindi cha mafanikio wakati hawakuwahi kuzungumza wakati mchezaji au wachezaji wakipambana.
Adui wa mpira wa Tanzania ni Watanzania wenyewe, tena kitu kibaya zaidi ni wale walio karibuni na jiko la maandalizi ya kila kitu kuhusiana na soka.
TFF:
Kwangu adui namba moja wa maendeleo ya soka nchini ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo linaendeshwa kama kampuni binafsi. Angalia leo wafanyakazi wake ndani wanalia kucheleweshewa mishahara lakini shirikisho hilo limeingiza mabilioni ya shilingi kutoka kwa wadhamini.
Kwangu adui namba moja wa maendeleo ya soka nchini ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo linaendeshwa kama kampuni binafsi. Angalia leo wafanyakazi wake ndani wanalia kucheleweshewa mishahara lakini shirikisho hilo limeingiza mabilioni ya shilingi kutoka kwa wadhamini.
Angalia mambo yanavyokwenda wakati wa uendeshaji, upangwaji wa ratiba, kuvurugwa, kuwekewa viraka, timu kuruhusiwa kwenda kushiriki mabonanza na kuachana na ligi na mambo rundo.
Nani anaweza kuwaeleza TFF, wanaamini Fifa ndiyo serikali yao, hawawezi kuwa na heshima kwa wadau wa soka nchini na kwa mfumo ulivyo hawawezi kuwafanya lolote kwa kuwa pia viongozi wao wana urafiki na viongozi wa juu serikalini, wanaweza kufanya wanachotaka kuendeleza kila upuuzi.
Leo utaona, uchaguzi wa vyama vya wilaya kama Temeke (Tefa) na Kinondoni (Kifa) umekuwa na figisu kubwa, kelele, wizi wa wazi na ubabe usio na kificho. Hii ni kwa kuwa tu kuna viongozi dhaifu wamepitwa na hawatakuwa na msaada na vigogo wa juu katika soka. Hivyo ni lazima wapatikane wanaotakiwa.
Angalia, sasa TFF inataka kufanya uchaguzi wa kila klabu ili iweze kupanga safu ya watu ambao watakuwa msaada kwenye uchaguzi, si faida kwa soka.
Viongozi wa juu wa soka, wanataka kujiwekea mazingira ya kushinda tena TFF msimu mwingine. Hivyo wangependa kupanga safu itakayokuwa msaada kwao, hapa hawaangalii nani ni msaada kwa mpira wa Tanzania. Halafu wanajiita ni baba wa mpira wa Tanzania, ujinga mtupu.
MWENYEKITI WA YANGA, YUSUF MANJI |
Yanga, Simba:
Hawa ndiyo vigogo wa soka nchini, hauwezi kuwakwepa hata kidogo na mashabiki na wanachama wao wengi ni wanaozipenda kweli klabu zao, lakini wako kwenye makundi mawili.
Kundi moja, kweli ni lenye mapenzi ya dhati kwa faida ya mpira, kundi jingine ni kundi maslahi na hili linahusika katika ubomoaji wa soka nchini.
Kundi maslahi, ndilo linalohusika na rushwa, kutisha viongozi au kupanga fitina zenye mlengo wa kuwapatia wao maslahi na si klabu. Wapo wanaoitwa ‘Makoma-ndoo’. Hawa ni tatizo kubwa na wameendelea kudumu, ni tatizo kubwa kabisa.
Viongozi wa klabu hizi wana nguvu kwa kuwa wana nguvu za watu nyuma. Wanavunja utaratibu, wanaendesha mambo wanavyotaka wao na hakuna anayewazuia.
Wao wanaamini wanasaidia maendeleo, lakini wanashiriki kwenye mambo mengi zaidi ya kuporomosha maendeleo na wanajua, lakini wanaendelea huku wakilia maendeleo hayapatikani.
Lakini ajabu kabisa, hata Azam FC, timu iliyoonekana kama mleta maendeleo, wameingia kwenye mkumbo nao wanapita njia za Yanga na Simba, sasa hakuna tofauti.
Azam FC sasa ni watu wa kulalamika, wanataka kupewa nafasi au kuonekana kama Simba au Yanga! Wanajiona ni wakubwa, wanataka kukuzwa na kulazimisha waonekane ni wakongwe, jambo sasa limegeuka tatizo na linawaporomosha. Sasa hawana tofauti kubwa kama ambavyo ilionekana.
Rushwa:
Waungwana, watu wanajaribu kuficha, soka ya Tanzania inaporomoshwa na rushwa. Tatizo limekuwa kubwa sana, leo waamuzi wanaona kupewa rushwa ni haki yao.
Mwamuzi kama hatapewa kitu katika mechi, ataona kama ameonewa. Wako wengi wanafanya hivyo na wanajua, watanielewa tu wakati wanasoma hapa namna wanavyocheza michezo yao ya uhamishaji fedha katika simu.
Hata upangwaji wa mechi, yaani mwamuzi huyu achezeshe mechi hii nako kunaweza kuwa sehemu ya zengwe kwa kuwa kunatakiwa mgawo fulani upitishwe.
Upangaji wa ratiba za ligi nao una figisu, nao unahusisha furaha ya watu fulani au maslahi yao binafsi. Nani anaweza kusaidia kupatikana maendeleo katika dimbwi la harufu na kichefuchefu cha rushwa kinachoendelea? Tena waamuzi wengine wanadhulumu hadharani kuzitetea timu fulani kwa kisingizio cha makosa ya ubinadamu.
Lakini wakati unazungumzia rushwa kwa waamuzi, wachezaji wenyewe pia wakiwa wanatuhumiwa tena katika jambo ambalo linaonekana ndani yake kuna uweli. Sasa hata viongozi wa TFF nao wana tuhuma hizo.
Tulielezwa kwamba suala lao liko Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea tena, suala limekwisha, ukiuliza sababu za msingi zitakuwa hazina tofauti na suala la kubebana kwa kuwa watu wanafanikiwa.
Waandishi wamekaa kimya wanahofia tena kuhoji, huenda hofu ya Takukuru ya vigogo kuingilia au kuhusika. Lakini ukweli chombo kama Takukuru kama kitakuwa hakina meno ya kushindwa kuwang’ata vigogo wanaoshiriki katika rushwa, halafu kinasubiri dagaa waharibu ili wakamatwe, ni uwajibikaji mwingine usio na misingi sahihi iliyojaa uzalendo na kufanikisha ukweli na usafi uliolenga kupigania mafanikio.
Viongozi wote wa soka wanajua rushwa ipo, inapita wapi, wahusika ni akina nani na njia ni zipi. Lakini wanaendelea kulalamika kila mmoja akitoa pasi kwingine. Imekuwa ni ile ishu ya ‘chukua chako mapema’. Dalili za kudumaza mchezo wa soka nchini zimeshaonekana, kilichobaki ni msiba.
Wadau wanalia mengi kuhusu mafanikio mabovu ya timu ya taifa, lakini wanajua madudu ndani ya soka. Mpira ndiyo sehemu kiongozi anaweza kufanya anavyotaka, akafuja fedha anavyotaka halafu mwisho akaishi anavyotaka hata kama ataondoka ndani ya soka.
Mchezo wa soka ni maslahi binafsi na si ya taifa. Kila mmoja anataka kwa ajili ya mafanikio yake, hivyo anafanya kwa ajili yake na familia yake pamoja na marafiki zake.
Wanaotakiwa kuthibiti vitendo vya rushwa nao wanaonekana wako taratibu, hawana haraka, huku wakijitapa kuwa wanaondoa tatizo. Wanaosema ukweli ndiyo adui namba moja, wanaosaidia uozo huo ndiyo watu bora na serikali ipo.
Serikali nayo ni sehemu ya tatizo kubwa kwa kuwa haishiriki katika maendeleo ya michezo nchini. Hata viwanja vya wazi vilivyotolewa kwa ajili ya maendeleo ya soka na michezo mingine vilitaifishwa na serikali ikashindwa kuvilinda. Lakini baadaye utasikia viongozi wao nao wanahimiza kuhusiana michezo.
Utaona kila kiongozi wa serikali anataka kuendeleza michezo wakati wa kampeni za uchaguzi. Eti kapeleka mipira na jezi jimboni na kwa kuwa wananchi ni watu wa kusahau, wanapokea kwa shangwe huku wakisahau unafiki na uzandiki wa juu kabisa wa viongozi hao. Wote wanaofanya ubabaishaji kwa manufaa yao ni maadui wa soka.
Kwingine soka linaendelea kwa kuwa watu wanafanya mambo kwa dhati wakilenga mafanikio ya soka. Hapa wanalenga mafanikio binafsi.
0 COMMENTS:
Post a Comment