June 13, 2016Na Saleh Ally
UKWELI ni jambo jema sana katika maisha hata kama utakuwa umeamua kuwatetea watu ambao unaamini ni wako au wale ambao unapaswa kuwatetea katika jambo lolote lile.

Kila Mtanzania ana haki ya kuwatetea wazawa kwa kuwa naye kama mzawa atatetewa na wengine. Hilo ni jukumu la msingi na linaingia katika kipengele cha uzalendo katika maisha ya kawaida.

Mimi ni muumini wa wazalendo, natamani kuona kijana kutoka hapa nchini akifanikiwa kuliko yule anayetokea nje ya nchi hii, acha niwe wazi tu ili nieleweke.

Lakini siwezi kuingia kwenye vita ya kumzuia kijana wa nje asifanikiwe kama namuona ana juhudi na maarifa, anajituma pia ni mtu ambaye amepania kufikia ndoto zake. Nitakachofanya nitamuunga mkono.

Nitakueleza kwa nini nitamuunga mkono, mimi ni muumini wa watu wanaojituma, watu wanaotaka kufanikiwa na wanapambana kwa vitendo badala ya maneno mengi na kulalamika kila kukicha. Hapo, uzalendo nauweka kando.

Kupitia Metodo, leo nimeona vizuri kujadili suala la wachezaji au wanasoka wazalendo katika nchi yetu ambao wamekuwa wakisonga kwa mwendo wa kusua na wengine wanalia kuwa wanavunjwa moyo au nguvu na viongozi wa klabu mbalimbali ambao wanaonyesha kuweka nguvu nyingi kwa wageni.

Kuacha viongozi waweke nguvu nyingi kwa wageni bila sababu zozote za msingi hasa kama wanaona wana uwezo mdogo, kweli haliwezi kuwa jambo la kuachiwa lipite hivihivi, tutalivaa na kupambana nalo na mara nyingi nimekuwa nikifanya hivyo. Napinga wachezaji wa kigeni kulipwa fedha nyingi kwenye Ligi Kuu Bara, huku wakipewa nyumba na marupurupu zaidi lakini uwezo wao unafanana na wazawa au kuwa chini kabisa. Hilo siwezi kukaa kimya hata kidogo.

Kinachoniudhi ni kwamba wakati wazalendo tunapambana kwa ajili ya kuwarekebisha viongozi ili watupe nguvu kwa vijana wazawa, vijana hao wanaendelea na mambo ya kijinga kabisa ambayo wao wanataka kuyegeuza ni sehemu ya maisha yao huku wakijua kweli ni ya kijinga.

Wachezaji au wanasoka wengi wazalendo wanaamini bangi ni sehemu ya mafanikio, wapo wanaoona mvuta bangi ndiye anayeweza kufanya vizuri katika soka, hili ni jambo la kijinga kabisa.

Wako ambao hawana nidhamu katika kazi yao, hawalali mapema, hawana muda wa kupumzika, hawajitumi mazoezini, hawawasikilizi walimu wao lakini ajabu wana ndoto za kufika mbali kwa maana ya mafanikio, huu ni ujinga mwingine wa juu kabisa.

Kulitetea taifa letu ni sehemu ya jukumu letu, lakini haitakuwa sahihi kuendelea kuwatetea wanaofanya mambo ya kijinga ambayo wanajua ni tatizo kwao na wakaendelea kufanya tena bila ya kuchoka, halafu tuendelee kuwalilia kwamba wanapunjwa au kuonewa, utakuwa ujinga zaidi.

Kuna kila sababu ya vijana wa Kitanzania ambao mnaamini soka ni ajira yenu kuanza kutengeneza nidhamu ya juu kabisa kuhusiana na kazi na lazima mjue, mnalipwa mishahara hadi Sh milioni moja na zaidi huku wale wanaofanya kwenye makampuni makubwa kama benki, makampuni ya simu hawawafikii mishahara yenu.

Lakini kwa kuwa wengi wenu hamjui thamani ya kazi yenu, mnaendelea kuichezea kazi huku mkiwa na nyimbo nyingi za kulalamika kuwa mnaonewa. Huenda ni kwa kuwa na sisi tunaendelea kuwatetea, acheni mambo hayo ya kijinga ili muweze kupiga hatua.

Vijana wengi wa Kitanzania wana vipaji vya juu kabisa michezoni. Lakini wamekuwa waoga kwenda kucheza nje ya Tanzania kwa kuwa wana hofu ya juu kuhusiana na nidhamu yao na aina ya maisha wanayoishi.

Acheni kulalama hovyo, fanyeni kazi kwa kujituma, kwa juhudi na maarifa. Pia lazima mjue, hata kama una kipaji kikubwa kumpita Lionel Messi na Cristiano Ronaldo halafu hauna nidhamu wala juhudi, utafeli tu. Hata tukutetee vipi, utafeli tu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV