June 22, 2016


Yanga ni kama imewazuga wapinzani wao TP Mazembe ya DR Congo baada ya kuamua kurejea kwenye jiji la Antalya, Uturuki kwa ajili ya kambi huku ikipanga kutua Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumapili.

Hiyo ni siku moja tangu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha timu hiyo Jerry Muro kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa timu hiyo ingerejea jana Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

Yanga inatarajiwa kuvaana na Mazembe Jumanne ijayo kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa walifungwana MO Bejaia ya Algeria bao 1-0, kabla ya kurejea Uturuki.

Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema itarejea usiku wa saa saba wa kuamkia Jumapili na moja kwa moja wataingia kambini kujiandaa na mchezo huo.

Saleh alisema, timu hiyo iliingia Uturuki jana saa 12:00 asubuhi wakitokea Algeria kuvaana na MO Bejaia na mara moja kuanza maandalizi ya mchezo huo pamoja na mshambuliaji mpya raia wa Zambia, Obrey Chirwa.

"Awali tulikuwa tupo kwenye mipango ya kurejea Dar mapema kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mechi na Mazembe, lakini uongozi umebadilisha mpango na badala yake tutarejea Uturuki kuendelea na maandalizi hayo.

"Timu itarejea huko Dar majira ya usiku wa kuamkia Jumapili saa saba na moja kwa moja tutaingia kambini kwa ajili ya mchezo huo, hivyo tukiwa huku Uturuki, ratiba ya mazoezi tumeibadilisha kidogo kwa kufanya mazoezi ya jioni pekee na siyo usiku kama mwanzoni tukijiandaa na mechi na MO Bejaia.

"Hiyo yote ni kuendana na hali ya Dar ambayo ni ya joto kali kama ilivyokuwa huku kuna jua na joto kali, hivyo kocha kashauri tufanye mazoezi kwa muda huo,"alisema Saleh.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans Pluijm alisema anachokifanya ni kuwatengeneza kisaikolojia wachezaji baada ya kupoteza mechi na MO Bejaia ili wasahau matokeo hayo yaliyopita.
"Siku zote ninapomaliza mechi moja, tunasonga mbele na kujiandaa na mechi nyingine inayofuata, hivyo tumeona makosa yetu tuliyofanya katika mechi iliyopita na badala yake ninayafanyia marekebisho makosa yaliyotokea.


"Kikubwa ninawasisitizia wachezaji wangu kutofanya makosa kama tuliyofanya kwenye mechi iliyopita ambayo yalitugharimu kwa wapinzani wetu kuyatumia makosa yetu na kutufunga, hivyo sitaki hayo yajitokeze tena mechi na Mazembe,"alisema Pluijm.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV