July 27, 2016

SEMWANZA
Simba tayari imekamilika katika mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara baada ya beki wa kati wa timu hiyo, Emmanuel Semwanza kurejea kikosini katika kambi ya timu hiyo huko mkoani Morogoro.

Semwanza aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Mwadui FC ya Shinyanga, alikuwa mchezaji pekee wa timu hiyo ambaye hajajiunga na timu hiyo kutokana na kufiwa na mama yake mzazi na hivyo kupata udhuru wa kuhudhuria mazishi mkoani Mbeya.

Akizungumza na Championi Jumatano, meneja wa timu hiyo, Abbas Ally, amesema kuwa Semwanza amejiunga na kikosi hicho rasmi juzi baada ya kuwa nje ya kikosi kwa takriban siku tano, hivyo sasa kikosi hicho kipo kamili katika maandalizi yao chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog.

“Kambi inaendelea vizuri, hakuna tatizo lolote zaidi amerejea Semwanza ambaye yeye alikuwa nje ya kikosi kutokana na msiba, hivyo sasa kikosi kimekamilika katika kuendelea na programu za mwalimu za kujiandaa na msimu mpya wa ligi,” alisema Abbas.

Mpaka mwisho wa wiki hii Simba itakuwa imetimiza wiki nne katika kambi hiyo ikiendelea kujifua na kuwajaribu wachezaji wa kigeni waliopo kikosini humo na kama wakifuzu waingie kandarasi za kuitumikia timu hiyo msimu ujao, lengo likiwa ni kurekebisha makosa ya kutoshiriki michuano ya kimataifa kwa misimu minne mfululizo. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV