Aliyekuwa nahodha wa Simba, Hassan Isihaka, ametamka kuwa kwa sasa hana timu ya kuichezea na yupo nyumbani tu.
Isihaka ambaye alitengeneza ukuta imara akiwa Simba akishirikiana na Mganda, Juuko Murshid, ametemwa nje ya kikosi cha Simba ambacho kimejichimbia mkoani Morogoro chini ya kocha wake Mcameroon, Joseph Omog kikijiandaa na msimu ujao wa ligi kuu.
Akizungumza kuhusiana naye, beki huyo anayechipukia alisema kuwa mpaka sasa amekuwa akikaa nyumbani tu kutokana na kutemwa na timu yake hiyo ambapo hakuna timu yoyote ile iliyomfuata kwa nia ya kumsajili.
“Nipo nyumbani tu, sina timu yoyote ya kuichezea mara baada ya kutemwa na Simba ambapo mpaka sasa hakuna timu yoyote ile ambayo imenifuata kwa ajili ya kunisajili kwa msimu ujao.
“Sijajua hatma yangu itakuwaje msimu ujao kwa sababu sina timu lakini naamini mambo yatakuja kukaa vizuri kabla ya dirisha la usajili kufungwa, timu zitakuja tu,” alisema Isihaka.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment