July 27, 2016


Kama wanatania, lakini Prisons wapo ‘siriaz’ baada ya kocha wao, Abdul Mingange kutamka wazi kuwa malengo yao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ni kuwa mabingwa na si kingine.

Mingange amepewa mkataba wa miezi sita ya kuinoa timu hiyo akichukua nafasi ya Salum Mayanga aliyetimkia Mtibwa Sugar. Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza ligi ikiwa ya nne huku Yanga wakifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Mingange alisema kila timu huwa na malengo ya kumaliza msimu ikiwa bingwa, hivyo hata wao wana malengo hayo na wanaamini watafanikiwa kwa hilo.

“Tupo kwenye maandalizi makali kuhakikisha tunafanya vizuri msimu ujao, malengo yetu ni kuwa mabingwa kwani kama timu msimu uliopita ilimaliza nafasi ya nne basi msimu ujao tunaweza kuwa mabingwa.


“Hayo ni malengo kwa kila timu na ndiyo maana sisi pia tumejiwekea hivyo, lakini pia nishukuru tu nimekuta kikosi kwenye hali nzuri na kwa hapa kilivyo sina haja tena ya kuongeza mchezaji, waliopo wanatosha kuipa timu ubingwa,” alisema Mingange ambaye aliwahi kuzinoa Mbeya City na Ndanda kwa vipindi tofauti.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV