July 25, 2016


Mgogoro wa nani zaidi kati ya pande mbili zinazopigania utawala wa timu ya Stand United ya Shinyanga limezidi kuchukua sura mpya ikiwa ni siku chache tu baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kuumaliza utata huo.

TFF hivi karibuni ilitangaza kuutambua uongozi wa timu hiyo uliowekwa madarakani na wanachama wa klabu hiyo baada ya kufanyika kwa uchaguzi ambao hapo awali ilidai kutoutambua.

Hali hiyo ilisababisha upande wa pili unaojiita Stand Kampuni kupinga hatua hiyo ya TFF kwa baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa timu hiyo kwenda mahakamani.

Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kwamba klabu hiyo hivi sasa ina timu mbili na zote zipo katika maandalizi makali ya kujiandaa na kivumbi cha Ligi Kuu Bara msimu ujao kinachotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20, mwaka huu.

Kikosi cha kwanza ambacho kipo chini ya uongozi unaotambuliwa na TFF, kipo mkoani Shinyanga kikijifua vilivyo chini ya makocha wa msimu uliopita, Mfaransa, Patrick Liewig pamoja na Athumani Bilali wakati kikosi kingine kilichopo chini Kampuni, kipo jijini Dar es Salaam kikijifua kwenye Viwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini hakina kocha.

Kutokana na hali hiyo, Championi Jumatatu lilizungumza na pande zote ili kujua nini hatima ya suala hilo na mtu wa kwanza alikuwa ni msemaji wa upande wa Kampuni, Muhibu Kanu ambaye alisema: 

“Suala hili bado halijaisha, tunamsubiri Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye arudi kutoka Dodoma ili aweze kulimaliza kwani TFF tunaona wameshindwa, kuhusu timu inaendelea kujifua katika Viwanja wa Chuo Kikuu, Dar es Salaam.”

Kwa upande wa Stand United inayotambuliwa TFF, msemaji wake Deo Kaji Makomba alisema: “Sisi tunaendelea na taratibu zetu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu, hivyo hayo mengine hayatuhusu kwani kila kitu TFF ilishakimaliza.”


Alipotafutwa Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema: “Sisi kwa upande wetu tunaitambua Stand United iliyosajiliwa kwa msajili wa vyama vya michezo, hivyo kama kuna Stand United nyingine basi hilo sisi hatulitambui lakini pia kama kuna timu zaidi ya mbili hilo pia halituhusu ila mwisho wa siku tutafanya kazi na Stand United tunayoitambua.”

SOURCE: CHAMPIONI 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV