Jana, Jumanne timu ya Yanga ilishuka uwanjani kupambana na Medeama katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika uliofanyika kwenye Uwanja wa Essipong Sports mjini Sekondi nchini Ghana.
Hata hivyo, wachezaji baadhi wa Yanga wameipigia saluti Medeama kwa fitna kabambe ilizowafanyia wakati walipotua Ghana kwa ajili ya mchezo huo ambazo zilifanya waingiwe na hofu kubwa ya kutekwa walipokuwa njiani wakitokea Accra kwenda Sekondi.
Wakizungumza na Championi Jumatano kwa nyakati tofauti wachezaji hao ambao ni, kipa Deogratius Munishi na mshambuliaji wa timu hiyo, Mrundi, Amissi Tambwe walidai kuwa baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Accra, ilikuwa ni usiku na walijua kutoka hapo kwenda Sekondi wangepewa ulinzi kutokana na umbali ambao wangesafiri kwa basi.
“Hata hivyo, hali haikuwa kama tulivyotarajia, tulisafiri usiku huo kwa basi tena kwa zaidi ya saa tano bila ya kuwa na ulinzi wa aina yoyote, hakika kila mtu ndani ya basi alikuwa akimwomba Mungu kila tulipokuwa tukifikiria hali ya usalama katika mataifa haya ya Magharibi.
“Akili zetu zilitawaliwa na hofu kubwa kwani tulikuwa tukipita sehemu nyingine zilikuwa ni mapori, hata hivyo hofu hiyo ilishuka baada ya kufika Sekondi na ndipo tulipoanza kutaniana huku baadhi yetu tukiona hali hiyo kama bonge la fitina ambalo wapinzani wetu walitufanyia kwa sababu walituvuruga kwa kiwango kikubwa,” alisema Dida.
Kwa upande wa Tambwe alisema: “Ilikuwa ni balaa tulifika tumechoka sana na hakuna mtu aliyekuwa akiamini kama tutafika salama Sekondi kutoka Accra ila tunamshukuru Mungu kwa hilo ila jamaa nimewakubali kwa fitna hiyo ya soka."
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment