July 1, 2016

RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI


Na Saleh Ally
MASHABIKI wa soka bado wanabaki na kumbukumbu ya kuingia bure katika pambano la Yanga dhidi ya TP Mazembe katika mechi ya Kombe la Shirikisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ulikuwa ni uamuzi wa uongozi wa Yanga kuamua kuwaingiza mashabiki bure kwa lengo la kupata mchezaji wa 12, yaani mashabiki ambao wangeiunga Yanga mkono kwa nguvu ili kuwamaliza mabingwa hao wa Afrika.

Kweli mashabiki wengi walijitokeza na mechi ikachezwa na kuisha salama ingawa kulikuwa na vurugu nje ya uwanja mashabiki wakitaka kuingia. Kizuri zaidi, hakukuwa na vurugu zozote za kuhatarisha usalama ndani ya uwanja.

Baada ya mechi hiyo ambayo Yanga ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya mabingwa hao wa Afrika. Tumerejea katika maisha ya kawaida na mjadala mkubwa ni kwa nini ilikuwa bure na inaonekana kabisa wako ambao hawakufurahishwa!

Walioamua watu waingie bure ni Yanga ambao wanaihudumia timu yao. Walisema wanafanya hivyo ili kupata sapoti kubwa ya mashabiki kwa kuwa walizitaka sana pointi tatu za Mazembe kwa kuwa walipanga kushinda mechi zote tatu za nyumbani ili kujiweka sawa baada ya kuwa wamepoteza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Mo Bejaia kule Algeria.

Wakati mechi hiyo imebaki historia, inaonekana kuna ugomvi unakuja. Kwani Tayari TFF imetangaza ndiyo itakuwa ikisimamia masuala ya mechi zote za Yanga likiwemo suala la ukataji wa tiketi, kitu ambacho ninaona ni kama kichekesho.

Leo TFF wamekumbuka shuka alfajiri, kwamba watakuwa wakiangalia wageni wanapotua nchini kuja kucheza na Yanga, wao wanaangalia kila kitu. Jiulize vipi hawakufanya hivyo kabla? Kama wanajua ni jukumu lao vipi waliacha, ni uzembe na kwa nini?

Pia wanasema wanasubiri ripoti ya kamisaa kuona kama kulikuwa na shida. Hizi inanipa hofu, kwamba kuna uwezekano hata wao wakafurahia kuona Yanga inalimwa faini ili kuthibitisha kwamba watu walioingia bure haikuwa sahihi.

Ukiangalia TFF wana kila sababu ya kukasirika kwa kuwa hawakupata mapato ambayo walitegemea kuingiza mlangoni na hili hawawezi kumdanganya mtu kama kweli walilifurahia.

Ndiyo maana hata wakati wa mechi hiyo, viongozi wengi wa TFF si kama tulivyozoea kuwaona uwanjani wakiingia kwa wingi hasa katika mechi kubwa. Siku hiyo, wengi wakawa na majukumu mengine.

Nafikiri hawapaswi kuonyesha wamekerwa sana na hiyo bure. Au hawana sababu ya kuanzisha au kufikiri kuanzisha uadui au kutaka kukomoana na Yanga ambao leo ndiyo wanaifanya TFF iendelee kujadili haya kwa kuwa imefikia ilipo.

Kama TFF itakuwa inatunishiana misuli na Yanga, hii itakuwa ni sehemu nyingine ya kuonyesha kuna tatizo kubwa kwa mzazi ambaye ni shirikisho hilo, kwamba anapenda sifa na hajali kuona wanaye wanaharibikiwa.

Kanuni ipi inasema Yanga ilikosea kuwapeleka watu waingie bure? Kama haipo na TFF iliona kuna tatizo kutokana na idadi kubwa iliyoingia, TFF ikae na Yanga na kuwaeleza ambacho wanaona hakikuwa sawa.

Vizuri ni kuepusha kuijaza Caf pumzi ili ione Yanga ilikosea sana. Fujo za nje ya uwanja, hakuna taarifa za matatizo makubwa. Na kama yalikuwepo kidogo, basi nini kifanyike kitu kuyamaliza ili wakati mwingine yasitokee.

Hii si mara ya kwanza Yanga kuamua mashabiki wake waingie bure katika mechi ya kimataifa. Kipindi uongozi wao haukuwa na misuli kama hii ya sasa.

Hili suala halihitaji hasira wadau, mashabiki walioingia bure ni Watanzania. Tushukuru walitoka salama, kama linaonekana lina makosa ndani yake, basi lijadiliwe kwa kiwango cha kujenga na si kulenga au kufikiri kukomoa au kuonyeshana. Onyesheni mnalenga kuendeleza mpira.

Kama Yanga wamekosea kutofanya biashara, basi vizuri muwashauri kibiashara na athari zake ni zipi na si “mimi ndiye mwenyewe”, haya yamepitwa na wakati sasa!0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV