July 1, 2016


KESSY

Na Saleh Ally
WAKATI mwingine ni vizuri kuzungumza kwa lugha inayoashiria umechukizwa au hufurahishwi ili wahusika waamue kama wanaweza kubadilika au la.

Maendeleo ya mchezo wa soka nchini, yanaangushwa na mambo mengi sana lakini kuu ambalo halijawahi kubadilika ni suala la ubinafsi.

Ubinafsi ambao unatafuna maendeleo ya soka nchini umegawanyika katika sehemu nyingi sana kwa kuwa wahusika wanaopenda kuongoza mchezo wa soka, wana miili iliyojengwa kwa ubinafsi.

Mmoja wa watunzi mahiri wa vitabu nchini Marekani katika miaka ya 1970, Richard Bach alikuwa akitumia msemo huu: “Kuepuka kujiangalia pekee na kujali wengine ni sifa ya uaminifu.”

Kama utakuwa unajijali wewe tu, maana yake wewe si mwaminifu kwa kuwa ni mtu unayetaka kujifaidisha, kujiendeleza na kuangamiza wengine bila ya kujali unachokiongoza au kukitumikia ni kitu cha watu na wewe ni sehemu ya waliobeba dhamana tu.

MWENYEKITI WA YANGA, YUSUF MANJI
Nimeanza hivi kwa kuwa ninataka kuwaeleza ukweli wa kuudhi viongozi wa klabu kubwa mbili za Yanga na Simba. Nawakumbusha kuwa si mali yao na wanapaswa kujua wako pale kwa idhini na wanapaswa kujua wanapaswa kuwa watendaji sahihi wa mambo na si watendaji wa hisia zao kutoka ndani ya mioyo yao kwa ajili ya kufurahisha nafsi zao.

Suala la beki Hassan Ramadhani maarufu kama Kessy linajulikana linavyokwenda. Kwamba amesaini mkataba mpya na Yanga, siku chache kabla ya kumaliza ule na Simba ambao ulikuwa umebakiza takribani siku 20 au chini ya hapo.

Simba, haimhitaji Kessy na wala haikuwa na mpango wa kumuongezea mkataba. Lakini sasa hachezi kwa kuwa kanuni zinaeleza hivi ni lazima apate barua kutoka Simba, hii ni kanuni.

Simba wameendelea kushikilia msimamo huo, lakini Yanga nao wameanza kuonyesha msimamo wao katika hilo. Wameandika barua wakiomba apewe nafasi ya kucheza kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hawakufanya hivyo kwa Simba!

Baadhi ya viongozi wa Simba, wanaeleza kuona kama wanadharauliwa na Yanga. Tayari wametishia msimamo wa wao kwamba Kessy anaweza kucheza wakati usajili utakapoanza hasa baada ya kupita katika kipindi cha pingamizi.

Meneja wa Kessy, Athumani Tippo ameona mambo ni magumu, tayari suala amelifikisha kwenye chama cha wanasoka, maarufu kama Sputanza ili asaidiwe.

Ukiangalia hapa, Kessy ambaye ni bwana mdogo, kijana wa Kitanzania ambaye anataka kuendelea kukuza kipaji chake anaendelea kuumia akisubiri kama atatokea mwenye nafsi ya huruma na mwenye nguvu amsaidie katika jambo ambalo unaliona limejaa utoto kabisa badala ya hali halisi.

RAIS WA SIMBA, EVANS AVEVA
Swali, Yanga wakiandika barua Simba na kuomba, watakosa nini na tatizo ni lipi hasa? Lakini Simba nao, wana haja gani ya kuendelea kutoa maneno yanayoonyesha wamepania na wanataka kukomoa?

Huenda Kessy aliwaudhi sana, naungana nao kwamba mwishoni, hakuonyesha nidhamu. Walikuwa wakilalama kwamba uhamaji wake ulionyesha viashiria kwamba hakuwa tayari kuonyesha ahsante kwa muda aliokuwa pale, badala yake aliondoka kwa mbwembwe.

Mimi yamewahi kunikuta hayo, kwa mtu niliyemlea tokea mtoto mdogo wa miaka 13, alipokua na kupata kazi, kwangu aliondoka kwa mbwembwe utafikiri kuna ugomvi au kapata kazi Marekani na hakuwahi hata kusema karibu nyumbani kaka. Huyu ni mtu uliyemlea kwa zaidi ya miaka 12. Mwisho nimesamehe kwa moyo wa dhati, nimemuacha anaendelea na maisha yake na sina shida naye hata kidogo. Kikubwa sina haja ya kujua anaendeleaje lakini sijazuia chochote au kuweka figisu katika maendeleo ya maisha yake.

Simba wanaweza kuachana na huo utoto wa kutaka nao kukomoa na wamuache aende. Ingawa bado ninaweza kumshauri Kessy kwamba lazima ajifunze kuonyesha uungwana. Hakupaswa kuwageuza Simba ni adui na kuonyesha uswahili na ujeuri huku hajui mbele nini kinafuatia.

Yanga nao, waonyeshe ukomavu. Badala ya mashindano ya nani mkubwa au zaidi au yupi ni maarufu sana au hajali. Basi wafuate kinachotakiwa ili Kessy aingie uwanjani.

Simba na Yanga, achaneni na furaha ya nafsi zenu wakati mkijua mnataka kuua kipaji cha kijana huyo. Fanyeni linalowezekana ili apate nafasi ya kucheza. Msiue vipaji vya vijana kwa kuwa mnataka kuonyesheana misuli, haina faida yoyote na mwisho kinachoonyesha ni ushindani wa kitoto kwa kuwa hauna faida hata kidogo.

1 COMMENTS:

  1. Simba na Yanga zinaweza zisiwe na Tatizo kubwa kwenye hili,mwenye tatizo kubwa ni mchezaji mwenyewe.Badala ya kuugeuza mpira kuwa ajira yake,alionyesha mapenzi ya dhahiri kwa Yanga kwa kufanya makosa ya makusudi kwa mwajili wake(Simba) ili kumhujumu na kuisaidia Yanga.Nani amesahau kadi za makusudi kabisa alizokuwa anazitafuta Kessy kwa lazima ili kuisababishia Simba pengo uwanjani?Ilifika hatua hadi timu nzima ya Simba wakiongozwa na golikipa Vincent waliugundua usaliti wake na akapokea mkong'oto toka kwa Vincent.Mchezaji wa aina hiyo aliyeihujumu Timu una haja gani ya kupoteza fedha na kununua kalamu na karatasi kumuandikia barua ya kumruhusu ahame?Asubiri muda wa pingamizi ukifika ataidhinishwa na TFF kwenda Yanga ambako alikuwa anakutumikia huku akiwa bado yupo Simba.

    Wachezaji limbukeni na washamba aina ya Kessy wapo wengi hapa nchini,ukiangalia hata mikao,picha na mambo mengine aliyokuwa anayafanya akiwa Kambini Uturuki na Yanga,yanamuonesha kuwa ni kijana wa aina gani,pamoja na kipaji alichonacho,amejawa na ushamba uliopitiliza na hajitambui.Hajuwi kuwa mapenzi yake yanaweza kuangamiza kipaji chake kizuri.Badala ya kuzilaumu Simba na Yanga,ni bora mwandishi ukachukua fursa ya kumuambia ukweli mchezaji ili ajitambue,vinginevyo atapotea mapema sana pamoja na kipaji kizuri alichonacho.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV