July 25, 2016


Wakati akiendelea na programu ya kutengeneza kombinesheni, Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amepanga kuanza na programu ya mazoezi ya kimbinu kwa wachezaji wake.

Hiyo yote ni katika kukisuka kikosi chake mara baada ya kumaliza programu ya fitinesi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, utakaoanza Agosti 20.

Mcameroon huyo anaendelea na programu hizo huku akiwa na baadhi ya nyota wapya waliowasajili kwa ajili ya msimu ujao ambao ni Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim, Mzamiru Yassin na Hamad Juma.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatatu limezinasa, kocha huyo hivi sasa amezielekeza nguvu zake huko kwa kuhakikisha wachezaji wake wanashika mbinu mbalimbali anazowapa.

Mtoa taarifa huyo alisema, kikubwa anataka kuona timu inacheza soka la pasi za haraka wakati timu ikiwa ina mpira ikishambulia kwenye goli la wapinzani.

Kocha huyo, pia amekuwa akisisitiza umakini wakati timu inapopoteza mpira, lakini kwa pamoja wote wanatakiwa kukaba kwa kuanzia washambuliaji, viungo na mabeki.

Aliongeza kuwa, kocha huyo bado anaendelea na mchujo wa baadhi ya wachezaji walio kwenye majaribio ya timu hiyo iliyoweka kambi yake mkoani Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu.

"Kocha hivi sasa anakwenda haraka na programu zake kutokana na kubanwa na ratiba ya ligi kuu iliyotolewa wiki moja iliyopita iliyopangwa kuanza Agosti 20, mwaka huu.

"Omog tayari amemaliza programu ya fitinesi na hivi sasa nguvu zake amezielekeza katika kutengeneza kombinesheni za wachezaji mbalimbali huku akiwapa mazoezi ya kimbinu.


"Mbinu hizo ni kucheza soka la pasi za haraka wakati timu ikiwa na mpira ikishambulia goli la timu pinzani, pia kukaba kwa pamoja pale timu inapopoteza mpira," alisema mtoa taarifa huyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV