July 25, 2016Licha ya Yanga kutoa sare ya 1-1 katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Medeama SC ya Ghana lakini Waghana hao wamekiri kuwa wana kazi kubwa ya kuwadhibiti mastraika wawili wa timu hiyo katika mechi ya marudiano itakayopigwa kesho, Sekondi, Ghana.

Waghana hao wameeleza wazi kuwa kati ya safu ambayo wanahitaji kujipanga zaidi ni safu yao ya ulinzi kwa ajili ya kuzuia usumbufu walioupata Dar katika mechi ya kwanza dhidi ya mastraika Mzimbabwe, Donald Ngoma na Mzambia, Obrey Chirwa.

Straika tegemeo wa Medeama, Bismark Oppong, ameliambia Championi kuwa Yanga ni timu nzuri lakini wamebaini kuwa wanabadilika zaidi pale mpira unapokuwa kwa mastraika wao hao, hivyo watajizatiti kuwazuia ili wasiwaletee shida wakiwa kwao.

“Ni kweli Yanga ni wazuri sehemu nyingi lakini mastraika wao wawili, yule Ngoma na aliyevaa namba 7 (Chirwa) ni wazuri sana. Hao ndiyo tunaotakiwa kucheza nao sana katika mechi yetu ya marudiano, hatutaki watusumbue Ghana, tukiwazuia hao, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Bismark.

Ukiachana na usumbufu aliouonyesha Ngoma katika mechi hiyo iliyopigwa hivi karibuni Uwanja wa Taifa, Dar lakini pia alifanikiwa kufunga bao la kuongoza katika dakika ya pili kabla ya Bernard Danso kuchomoa bao hilo dakika ya 18.

Tayari Yanga ambayo itamkosa beki wake Mtogo, Vincent Bossou katika mchezo wa marudiano kutokana na kuwa na kadi mbili za njano, imeshawasili Ghana tangu juzi Jumamosi. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV