July 11, 2016


Uongozi wa Yanga umeendelea kukaa kimya suala la Msemaji wake Jerry Muro kufungiwa mwaka mmoja na kamati ya maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini unajua unachokifanya.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga, zimeeleza uongozi umekuwa ukisubiri TFF kutoa ile hukumu ya Muro kufungiwa mwaka mmoja kujihusisha na masuala ya soka kwa madai kuipinga na kuishambulia TFF kwenye vyombo vya habari.

“Uongozi hauwezi kuzungumza kuhusiana na Muro kwa sasa, lakini una msimamo wake pia. Lakini unabaki kimya kwa kuwa kamati imekuwa ikijikanyaga kutoa hukumu.

“Lazima kuwe na maandishi kuhusiana na hukumu, akabidhiwe Muro na kopi iende Yanga. Lakini tokea wametangaza hadi leo kimya, jambo ambalo linaufanya uongozi ubaki kimya,” kilieleza chanzo.

Lakini wakati uongozi wa Yanga umekaa kimya, kumekuwa na taarifa kwamba hukumu imechelewa kutolewa kwa maandishi kwa kuwa Muro aliikosoa kwenye vyombo vya habari.


“Nafikiri wanataka waitie viraka kabla ya kuitoa, huenda wanataka ikitoka ijibu hoja zote za Muro ambazo aliwabana baada ya kuwa wamemfungia, ndiyo maana inazidi kuchelewa,” kilieleza chanzo hicho.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV