August 17, 2016

Kuelekea mchezo wa leo Jumatano wa Ngao ya Jamii kati ya Azam dhidi ya Simba, beki wa Azam, Aggrey Morris, ameshusha presha kikosini hapo baada ya kupona majeraha ya kifundo cha mguu yaliyokuwa yakimsumbua.

Aggrey ambaye tangu juzi alikuwa akifanya mazoezi na wenzake, kuna asilimia kubwa ya kuwavaa Yanga leo endapo tu ataonekana yupo tayari kwa mechi, lakini beki mwenzake, Pascal Wawa anayesumbuliwa na maumivu ya goti, hatacheza kwani bado hajapona.

Daktari wa timu hiyo, Twalibu Mbaruku, ameliambia gazeti hili kuwa, Aggrey ameungana na wenzake kwenye mazoezi na kuna uwezekano wa kucheza leo, lakini Wawa wamempa zaidi wiki mbili kabla ya kurejea rasmi uwanjani.

“Aggrey amefanya mazoezi asubuhi na wenzake na anaendelea vizuri, tutaangalia zaidi afya yake kama kuna uwezekano wa kucheza basi atacheza, Wawa yeye tumempa wiki mbili za kujiweka sawa kabla ya kurudi rasmi uwanjani,” alisema Mbaruku.

Awali, Kocha Mkuu wa Azam, Mhispania, Zeben Hernandez, alikuwa na wasiwasi juu ya kuwakosa mabeki wake wote hao wawili, lakini kwa sasa presha imeshuka kwani matumaini ya kumtumia Aggrey yamerejea.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV