August 12, 2016

DALALI


Na Saleh Ally
UONGOZI wa Klabu ya Simba umeanza ujenzi wa uwanja wao kwa takribani mwezi sasa. Ujenzi ni ule wa Uwanja wa Bunju ambao utakuwa wa kwanza kumilikiwa na klabu hiyo.

Simba itaanza kumiliki uwanja huo ndani ya miezi miwili kama kila kitu kitakwenda vizuri. Jambo ambalo litamaliza ‘ujinga’ waliokuwa nao Simba miaka nenda rudi.

Kama kila kitu kitakwenda katika mpangilio mzuri, basi Simba watamiliki uwanja wao, angalau wa mazoezi baada ya kuishi kwa miaka 80 bila kuwa nao.

Nimeandika sana kuelezea ambavyo nimekuwa nikishangazwa na Simba au kaka zao Yanga kutokuwa hata na uwanja wa mazoezi tu wakati wao kazi au biashara yao ni mpira.

Mara nyingi nimetolea mfano kuwa Yanga ni sawa na Mangi ambaye ni muuza duka, lakini hana sehemu ya kufanyia maandalizi ya biashara yake.

Kila ukifika wakati basi anakurupuka tu. Kamwe hawezi kulingana na Mangi aliyejipanga na kuziweka bidhaa zake katika mpangilio mzuri.

Kwa miaka 80, Simba imekuwa na wenyeviti zaidi ya 15 na utaona kila mmoja anaweza akawa sifa yake lakini katika kuondoa aibu hii ya uwanja, nianze na pongezi ya uongozi wa sasa wa Evans Aveva na wenzake, angalau wamepata fedha wakaona uwanja ni jambo muhimu.

Uwanja umekuwa ni ugonjwa wa muda mrefu na viongozi wengi walishindwa kuuponya na mwisho wake wakati wanaondoka wakamaliza kwa hadithi zisizokuwa na kichwa wala miguu.

Pamoja na kuupongeza uongozi wa sasa wa Simba, hakika niseme shujaa na ikiwezekana uwanja huo unapaswa kupewa jina lake na kuwa Dalali Stadium ni Field Marshal, Hassan Dalali.
Dalali ni wale wazee wa zamani wa Msimbazi, aliyeshika nyadhifa kadhaa kabla ya kuwa kiongozi wa juu wa Simba. Anayejulikana kuwa ni mwenye mapenzi kweli na klabu hiyo.
Anajulikana kwa kutokuwa na makuu, lakini mwenye mipango na huenda alikuwa akidharaulika kwa kigezo kwamba hajaenda shule kwa kiwango cha kuitwa msomi, lakini hili la uwanja, litabaki kuwa kumbukumbu ya milele katika klabu hiyo.

Dalali ndiye aliununua Uwanja wa Bunju ambao Simba leo wameamua kujenga. Aliununua baada kuamua kuanzisha tamasha, akalipa jina la Simba Day na baada ya hapo, sehemu ya mapato akanunua uwanja.

Dalali angeamua kuzila tu hizo fedha na leo hakuna ambaye angemkamata, Simba pia isingekuwa na uwanja na uongozi wa sasa wala usingepata sehemu ya kujenga uwanja huo leo.

Alichofanya Dalali si jambo dogo, kwani hata Simba Day aliyoianzisha imekuwa sehemu ya chanzo cha mapato kwa Simba na nikukumbushe, hakuna kijana au wale mnaoamini wasomi wakiwemo waliofika vyuo vikuu wamewahi kufanya uthubutu alioufanya Dalali ambaye anaonekana si msomi.

Akili ya Dalali, inaonekana ni kuwa ya kizamani. Ya wazee kama wale wa Simba au Yanga. Ambao walipoanzisha klabu, walipambana zikawa na makao makuu na majengo yake.

Utaona viongozi wa zamani ndiyo walifanya makubwa kuliko wale wa sasa ambao wana mipango mingi mdomoni na utekelezaji mkubwa kama ilivyokuwa kwa viongozi wa zamani ambao wengi wao walionekana si wasomi.

Akili ya kizamani wa Dalali imefanya mambo makubwa sana. Imeonyesha namna maneno yanavyoweza kuwekwa kwenye utekelezaji, namna mtu anavyoepukana na kusemasema na kuingia kwenye kundi la watendaji.

Ninaamini kama Simba na klabu nyingine kongwe kama Yanga, zitaacha tabia ya kuamini wazee hawana lolote, basi wanaweza kuendelea kuwa msaada.
Kingine kikubwa ni kwa wazee nao kujiamini na kutohofia vijana ni wasomi sana, wanajua mengi na wao hawawezi kulingana nao, badala yake kama wana mawazo jenzi, basi wayatoe na kusaidia mwenendo wa klabu zao.

3 COMMENTS:

  1. Hongera sana simba na mungu azidi kuwapa weledi wa kuangalia manufaa ya timu kwanza for the coming generation

    ReplyDelete
  2. unamzungumzia Dalali kama Taasisi lakini kama Decision maker

    ReplyDelete
  3. unamzungumzia Dalali kama Taasisi lakini kama Decision maker

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV