August 12, 2016




Na Saleh Ally
LIGI Kuu England ndiyo maarufu zaidi katika mchezo wa soka duniani. Kila mpenda soka angependa kushuhudia michezo yake.

Unajua, kila anayependa kushuhudia michezo hiyo, zaidi angependa kutulia akishuhudia mechi za moja kwa moja maarufu kama “live”.

Mechi live ni kama madini, kwani upatikanaji wake kutokana na mfumo wenyewe zinakuwa ghali sana na masikini wengi wamekuwa wakisumbuka kupata bahati ya kuzishuhudia kwa kuwa wasambazaji nao huzisambaza kwa bei ya juu kulingana na wanavyozipata.

Kwamba wahusika wakuu ambao ni wasimamizi wa ligi hulipwa fedha nao huzilipa klabu. Wao huingiza fedha kupitia makampuni ya runinga ambayo hurushwa sehemu mbalimbali duniani.

Wanavyokuwa ghali wasimamizi wa ligi hiyo ili wapate fedha za kuzilipa timu, ndivyo nao wanavyozilazimu kampuni za televisheni zinazosambaza, kuwauzia wateja wao kwa bei ya juu matangazo hayo ya live.

Watanzania wengi ni masikini, si rahisi kulinganisha kipato chao sawa na wale wa England au kwingineko duniani lakini mapenzi ya mpira, hayachagui masikini wala tajiri, kila mmoja anapenda kwa kiasi anachoridhika nacho.

Watanzania wengi wangependa kujua mwendelezo wa ligi hiyo na wanachotaka ni ‘kushea’ utamu huo kwa wakati mmoja na watu wa England na kwingine duniani. Live wakati wakishuhudia England, basi Tanzania nao wanashuhudia na kushangilia pamoja. Hata wasionazo, wanaweza kuliwazwa na soka, utamu wake ni furaha ya wengi sana.

Kampuni ambayo inaonyesha Premier League kwa uhakika hapa nyumbani ni DStv kupitia SuperSport lakini wapenda mpira wengi wamekuwa wakilalamika kuwa ni ghali sana. DStv nao wanasisitiza wangependa kuona kila mpenda soka anashuhudia ligi hiyo, tatizo ni gharama ndiyo zinawabana.

Kadiri siku zinavyosonga mbele, wamekuwa wakizidi kuteremka na kutafuta mbinu kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata nafasi ya kuona mechi za Premier League Live.

Safari hii DStv na msemo wao mpya wa “Hainaga Shobo Tunashangiliaga”, mbinu zao zinaonekana kuwa ni za dhati na mfano kabla ya kuanza kwa msimu wa 2016-17 ambao unaaminika kuwa, utakuwa mtamu zaidi ya mcharo, Multichoice Tanzania wametangaza hadi wale wanaolipia king’amuzi kidogo cha Sh 23,500 kwa mwezi nao wataona mechi live.

Wao wanaamini mechi hizo ni chaguo la wengi, lakini bado watakaolipa zaidi watakuwa wakifaidika zaidi kwa kuona mechi nyingi zaidi kulingana na mpangilio na ukubwa wa vifurushi.

Raha zaidi ni kwamba katika mechi 380 za msimu mzima wa Premier League, SuperSport itakuwa live hewani katika mechi 300 ambalo ni burudani maradufu kwa wapenda soka. Tena wameongeza zaidi kupitia Ligi Kuu ya Hispania maarufu kama La Liga kwani kwa ligi zote hizo mbili, zitakuwa mechi 760.

Kwa kuwa mara kadhaa tumekuwa tukiwakosoa Multichoice Tanzania kupitia DStv, kwamba lazima waangalie gharama kutokana na kipato cha wapenda soka wengi, safari hii tunaweza kuwasifia na kusema wameonyesha wanajali.

Wameonyesha wanajali kwa kuwa wametenga aina nyingi ya vifurushi lakini pia wameweza kushusha gharama hadi Sh 23,500 hapa napo wanaweza kuona soka tena Live, hili ni jambo jema.

Huenda ni wakati wa mashabiki wa soka, kuwaunga mkono, kununua ving’amuzi kwa wingi na kama wataweza kupata faida, huenda wanaweza kuona ni nafasi nzuri ya kuangalia namna wanavyoweza kupunguza gharama zaidi au kuongeza mechi nyingi zaidi kwa wale watakaolipa.

Lazima tukubali kuwa Multichoice Tanzania wanafanyabiashara, hivyo kama wataingiza faida wanaweza kuwa tayari wengi wapate zaidi nafasi ya kuona mechi za ligi hiyo.

Kama watapata hasara kwa watu kutojitokeza zaidi. Nao wanaweza kuzidi kukaza kamba na kurudi katika utaratibu ambao awali ulionekana ni tatizo na huenda uliwezesha wachache kuona mechi hizo. Hivyo vizuri kuwaunga mkono zaidi ili wawe msaada zaidi.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chance ambaye ni mzalendo wa kwanza kushika cheo hizo (si kukaimu), amesisitiza suala hilo kwamba huenda wataendelea kupanga mikakati ya kuhakikisha Watanzania wengi wapenda soka wanapata nafasi zaidi ya kushuhudia mechi hizo.

Pamoja na Premier League na La Liga, DStv bado wana mechi nyingi za michuano maarufu au mikubwa kama FA Cup, Capital One (yote kutoka England), Spanish Super Cup, Copa Del Rey na German Cup hivyo kuwafanya kuendelea kuwa wakongwe wanaotoa nafasi kubwa ya burudani katika mchezo wa soka, kuliko wengine wote.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic