Baada ya kukitazama kikosi chake kwa dakika 180 za mechi za awali za ligi kuu, kocha Joseph Omog wa Simba ameamua kuja na mbinu mpya kabisa kwa kutoa mafundisho maalum kwa kila idara kwa ajili ya kukijenga kikosi chake ili kuweza kuendana na upinzani wa ligi kwa kuwafanyisha mazoezi wachezaji wake kwa mafungu.
Hadi sasa Simba imeshacheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara ikiwemo dhidi ya Ndanda FC na JKT Ruvu ambapo moja ya mikakati ya kocha huyo ni kuhakikisha wanafanikiwa kushinda kila mechi watakayocheza.
Omog amefunguka kwa kusema, ameamua kuwafundisha kwa mafungu wachezaji wake kuhakikisha wanakuwa imara zaidi na kuleta ushindani kwenye ligi.
“Hii ni programu ni endelevu kwa wachezaji wangu kwa kuwa nafanya hivi kwa nafasi tofautitofauti na nina wiki sasa tangu nianze hii programu, nabadili wachezaji siku nyingine nawapa mazoezi maalumu viungo, siku nyingine mabeki pamoja na washambuliaji, inategemea na programu niliyoipanga siku husika.
“Lengo langu ni kuwaweka fiti na kufanya kila idara ikae sawa, pia nahitaji washambuliaji wangu wawe makini katika kufunga, hasa katika kipengele cha umaliziaji ambalo ndilo tatizo kubwa lililopo kwa sasa.
“Nahitaji kuwa na kikosi bora na chenye ushindani kwenye ligi kwa kuwa tunahitaji kufanya vizuri katika kila mechi,” alisema Omog.
0 COMMENTS:
Post a Comment