RAHIM (WA TATU KULIA MSITARI WA NYUMA) AKIWA NA KIKOSI CHA JKT. |
Beki wa JKT Ruvu ametoa kauli tata ambayo itawatibua Wanamsimbazi, amesema staa wao Laudit Mavugo ni wa kawaida tu na wala hatishi kama ilivyo kwa Donald Ngoma wa Yanga.
Beki huyo wa kati, Rahim Juma, ametoa kauli hiyo baada ya kufanikiwa kuizuia safu ya ushambuliaji ya Simba iliyo chini ya Mavugo kufunga bao lolote katika mchezo wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, juzi Jumamosi.
Juma aliwadhibiti vilivyo washambuliaji wa Simba, Mrundi, Mavugo na Muivory Coast, Frederic Blagnon katika mechi hiyo.
Alisema Mavugo na Blagnon ni washambuliaji wa kawaida sana na wanakabika kirahisi kutokana na kutokuwa na uwezo mkubwa wa kuficha mpira kama ilivyo kwa Ngoma ambaye anajua kuficha mpira, lakini pia ana kasi kubwa pamoja na nguvu kushinda washambuliaji hao wa Simba.
“Nilipokuwa nikisikia Mavugo akisifiwa sana katika vyombo vya habari nilijua kuwa ni hatari zaidi kushinda Ngoma, lakini baada ya jana kukutana naye pamoja na Blagnon, nimewaona kuwa ni wachezaji wa kawaida tu, hawana tofauti sana na washambuliaji wetu wa hapa nchini ila wanachowazidi ni jina tu kuwa wanatoka nje ya nchi lakini uwezo wa soka hauna tofauti.
“Mshambuliaji ambaye kidogo ukikutana naye uwanjani inabidi utumie nguvu na akili ya ziada kumkaba ni Ngoma wa Yanga, huyo ndiye naweza kusema kuwa hakuna kama yeye kwa sasa hapa nchini lakini Mavugo na mwenzake huyo, viwango vyao ni vya kawaida, hata Ibrahim Ajib ni mzuri kushinda wao,” alisema Juma ambaye msimu uliopita alikuwa akiitumikia African Sports ya mkoani Tanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment